Moscow: Marekani inachuma pesa kutokana na vita vya Ukraine
Msemaji wa Kremlin amekosoa himaya ya kifedha na kisiasa ya Washington kwa serikali ya Kiev na kusema: Marekani inapata pesa kwa kuuza rasilimali zake za nishati za bei ya juu kwa watu wa Ulaya walioathiriwa na vita.
Dmitry Peskov amesisitiza kuwa Marekani inawanyang'anya pesa watu wa Ulaya kwa kisingizio cha vita vya Ukraine, na Washington inachuma pesa kwa kutumia vibaya kila fursa inayopata."
Hii ni katika hali ambayo Rais Mpya wa Marekani Donald Trump juzi Jumatano alisema kuwa atatoza kodi zaidi, ushuru na kuweka vikwazo kwa kila kitu kitakachouzwa na Russia kwa Marekani na kwa nchi nyinginezo iwapo hakuna mapatano yatakayofikiwa kwa ajili ya Ukraine.
Msemaji wa ikulu ya Russia (Kremlin) pia alikumbusha kuhusu hotuba ya juzi ya Donald Trump aliyesema hatafuti njia za kuisababishia madhara Moscow, kwa sababu anawapenda watu wa Russia na amekuwa na uhusiano mzuri na Rais Vladimir Putin na kusema: Kremlin inafuatilia kwa makini matamshi na taarifa zote, na iko tayari kwa mazungumzo yaliyo sawa na kwa kuheshimiana pande mbili.