Matukio ya Uturuki na mashariki mwa Mediterania
(last modified Mon, 17 Aug 2020 13:28:13 GMT )
Aug 17, 2020 13:28 UTC
  • Matukio ya Uturuki na mashariki mwa Mediterania

Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uturuki na Marekani wamekutana katika Jamhuri ya Dominican na kujadiliana kuhusu matukio ya eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania na nchi ya Libya.

Mawaziri hao wawili wametoa taarifa wakisema kuwa: Katika mkutano huu pande mbili zimesisitiza udharura wa kupunguzwa mivutano katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania.

Hapana shaka yoyote kwamba, machafuko ya ndani nchini Libya na taathira zake katika eneo la mashariki kwa Bahari ya Mediterania vimetayarisha mazingira ya kujitokeza ushindani baina ya madola kadhaa kwa ajili ya kuwania utajiri wa nishati na kupanua satua na ushawishi wao katika eneo hilo. Kwa maneno mengine ni kuwa, eneo la mashariki mwa Mediterania na utajiri wake wa nishati limekuwa miongoni mwa mambo muhimu sana yanayozishughulisha nchi nyingi. Uturuki, Qatar, Misri, Ugiriki, Imarati na Syprus ni miongoni mwa nchi zinazolipa umuhimu mkubwa suala hilo, na kila moja kati ya nchi hizo inataka kuibuka kidedea katika kinyang'anyiro hicho. Katika mkondo huo harakati za Uturuki katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania na operesheni za meli za nchi hiyo za kutafuta gesi katika eneo hilo zimezusha hasira na wasiwasi baina ya nchi za kanda hiyo. Kuwepo majeshi ya Uturuki nchini Libya pia kumezidisha mivutano ya Tripoli na baadhi ya nchi jirani za kandokando ya Bahari ya Mediterania.

Mivutano ya eneo la Bahari ya Mediterania ilianza kushadidi mwaka jana baada ya Uturuki, Ugiriki na Syprus kuanzisha harakati za kutafuta na kuchimba gesi katika eneo hilo. Suala hili sasa limechochea mivutano baina ya pande mbili hasimu. Kwa mfano tu siku chache zilizopita Umoja wa Ulaya ulitangaza kuwa: Mpango wa Uturuki wa kuchimba mafuta na gesi katika maeneo ya pwani mwa kisiwa cha Syprus umezusha wasiwasi baina ya nchi za eneo hilo. Umoja wa Ulaya umetahadharisha kuwa, hatua hiyo ya Uturuki imezidisha mivutano baina ya nchi hizo mbili na haikubaliki.

Josep Borrell

Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell Jumapili iliyopita aliitaka Uturuku isitishe shughuli za kuchimba gesi mashariki mwa Mediterania. Borrell alisema: "Nawataka viongozi wa Uturuki wasimamishe mara moja harakati hizo na kuanza mazungumzo mapana zaidi na Umoja wa Ulaya." Wakati huo huo Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya alisisitiza kuwa: Hatua yoyote ya Uturuki ya kuanza tena kuchima gesi na mafuta katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania itazidisha mivutano katika eneo hilo.

Katika upande mwingine mchambuzi wa masuala ya Uturuki, Fateh Ozkan, anaamini kuwa: Kukaa kimya Uturuki kuhusiana na hali ya Libya na mashariki mwa Bahari ya Mediterania kutaathiri moja kwa moja jiografia ya kisiasa na stratijia za Ankara. Kwa msingi huo hatua ya Uturuki ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kuchimba gesi na mafuta katika eneo la baharini na Libya imeainisha mipaka ya baharini ya Ankara katika eneo la mashariki mwa Mediterania."

Meli ya kuchimba gesi ya Uturuki

Novemba mwaka jana Uturuki na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya zilisaini makubaliano ya masuala ya baharini na ushirikiano wa pande mbili katika masuala ya kiusalama na kijeshi. Mkabala wake, Misri na Ugiriki pia zilisaini makubaliano kama hayo kuhusu eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania, suala ambalo limezidisha utata katika hali ya mvutano inayotawala eneo hilo.

Kwa sasa nchi za Ugiriki, Misri, Imarati, Saudi Arabia, utawala wa kibaguzi wa Israel, Russia na Ufaransa zinataka kutimiza malengo yao nchini Libya na katika Bahari ya Mediterania kwa kumuunga mkono jenerali muasi, Khalifa Haftar. Katika upande wa pili Uturuki, Italia na Qatar zinaisaidia Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, hitilafu za sasa baina ya nchi zinazowania maslahi katika Bahari ya Mediterania yumkini zikazitumbikiza pande mbili katika vita visivyo na tija. Hii ni pamoja na kuwa, kujiingiza madola makubwa ya kibeberu kama Marekani katika mvutano huo, hususan baada ya mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na mwenzake wa Uturuki, kutachochea zaidi hitilafu zilizopo na kuzidisha matatizo na mivutano baina ya nchi hizo.

Tags