Pakistan yasikitishwa na Charlie Hebdo kumvunjia tena heshima Mtume SAW
Pakistan imelaani vikali uamuzi wa jarida linalochapishwa nchini Ufaransa la Charlie Hebdo wa kuchapisha tena vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW).
Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imesema: Tunalaani kwa nguvu zote uamuzi wa jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo wa kuchapisha tena kibonzo kinachomtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW).
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kitendo hicho cha kichochezi na kinachogusa nyoyo na hisia za mabilioni ya Waislamu kote duniani hakipaswi kuhalalishwa kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan imeeleza bayana kuwa, vitendo vya namna hiyo vinarejesha nyuma jitihada za kimataifa za kuhakikisha kuwa jamii ya wanadamu inaishi kwa utangamano, maridhiano, amani na maelewano bila kujali tofauti zao za kidini.
Inaarifiwa kuwa kwa mara nyingine tena jarida hilo la Kifaransa la Charlie Hebdo limeamua kwa makusudi kuwafanyia kejeli na istihzai Waislamu na dini tukufu ya Uislamu kwa kuchapisha vibonzo hivyo leo Jumatano, siku ya kuanza kwa kesi dhidi ya watuhumiwa wa shambulizi dhidi ya makao makuu ya jarida hilo Januari 7 mwaka 2015.
Hii si mara ya kwanza kwa jarida hilo linalochapishwa nchini Ufaransa kukanyaga thamani za kidini pamoja na uhuru wa imani na itikadi za watu wengine, kwa kuwatusi Waislamu na matukufu yao.
Jarida la Charlie Hebdo limeshapicha mara kadhaa katuni na vibonzo dhidi ya dini hususan dhidi ya dini tukufu ya Uislamu na Mtume wake Muhammad (S.A.W) kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, licha ya kukabiliwa na malalamiko makubwa ya Waislamu nchini Ufaransa na katika pembe mbalimbali za dunia.