Oct 03, 2020 02:42 UTC
  • Mamia ya nafasi za ajira zapotea kwa corona Amerika ya Latini

Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) limetangaza habari ya kupotea zaidi ya fursa milioni 34 za kazi kutokana na wimbi la maambukizi ya kirusi cha corona katika eneo la Amerika ya Latini.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema, eneo la Amerika ya Latini na Caribbean limepoteza fursa milioni 34 za kazi na hivyo limetumbukia kwenye mgogoro mkubwa ambao haujawahi kutokea katika soko la ajira. Limesema, takwimu hizo zimetolewa baada ya kufanyiwa uchunguzi hali ya ajira ya kipindi cha miezi mitatu ya awali ya mwaka 2020 katika nchi 9 za Amerika ya Latini zinazounda karibu asilimia 80 ya ajira za eneo hilo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukanda wa Amerika ya Latini na Caribbean umekumbwa na upungufu wa asilimia 20.9 ya fursa za kazi katika miezi mitatu ya awali ya mwaka huu ikilinganishwa na wastani wa asilimia 11.7 ya maeneo yote duniani. Hivyo eneo hilo ndilo lililodhuriwa zaidi na ugonjwa wa COVID-19 ikilinganishwa na maeneo mengineyo.

Eneo la Amerika ya Latini hivi sasa ndicho kitovu cha ugonjwa wa COVID-19

 

Nalo Shirika la Kimataifa la Misaada ya Kibinadamu liitwalo OXFAM hivi karibuni lilitangaza kuwa, kwa uchache wakazi milioni 52 wa Amerika ya Latini wametumbukia kwenye ukata mkubwa kutokana na mgogoro wa corona.

Sasa hivi eneo la Amerika ya Latini ndicho kitovu cha ugonjwa wa COVID-19 duniani. Takwimu zinaonesha kuweko ongezeko kubwa la vifo na maambukizo ya corona katika eneo hilo kwenye kipindi cha miezi ya hivi karibuni.

Tags