Maelfu waandamana Israel dhidi ya Netanyahu licha ya katazo
Maelfu ya Waisraeli wamefanya maandamano ya kumtaka Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu ajiuzulu kwa madai ya ufisadi na kushindwa kwake kulishughulikia janga la corona.
Katika maandamano hayo ya wiki ya 15 mfululizo, waandamanaji hao wamejitokeza kwa wingi kushiriki na kupuuza sheria kali iliyopasishwa hivi karibuni kwa ajili ya eti kudhibiti wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona.
Maandamano hayo ya jana usiku na leo Jumapili yamefanyika siku tatu baada ya Bunge la utawala huo haramu kupasisha sheria inayokataza watu kuandamana zaidi ya kilomita moja kutoka katika majumba yao.
Wadadi wa mambo wanaitakidi kuwa, sheria hiyo haikupasishwa kwa lengo la kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona kama inavyodai serikali ya Tel Aviv, lakini inakusudia kupunguza wimbi la maandamano hayo ya miezi kadhaa sasa dhidi ya Netanyahu.
Katika miezi ya hivi karibuni Israel imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ambayo yanamtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ajiuzulu kutokana na kile wanachosema waandamanaji kwamba, ni kushindwa kwake kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
Maandamano hayo yanafanyika kila Jumapili na kuhudhuriwa na maelfu ya watu. Netanyahu na baraza lake la mawaziri wanalaumiwa kwamba, badala ya kutanguliza mbele matatizo ya kiafya na kiuchumi yanayoisumbua Israel kwa sasa, wameng’ang’ania kusukuma mbele gurudumu la mipango ya kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.