Muuaji wa George Floyd aachiliwa huru nchini Marekani + Video
Afisa mzungu wa polisi wa Marekani ambaye alimuua kikatili na kinyama Mmarekani mwenye asili ya Afrika, George Floyd na kuzusha maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi dunia nzima, ameachiliwa huru kwa dhamana huko Marekani.
Shirika la habari la Associated Press limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, afisa huyo katili anayejulikana kwa jina la Derek Chauvin, aliachiliwa huru jana kwa dhamana ya dola milioni moja.
Afisa huyo mzungu alitiwa mbaroni tarehe 31 Mei mwaka huu kwa kosa la kumuua kikatili George Floyd katika mji wa Minneapolis huko Minnesota, magharibi mwa Marekani.
Mkanda wa video ulioenea sana katika mitandao ya kijamii, ulimuonesha afisa huyo mzungu wa polisi akimdidimiza kwa goti hadi kumuua Mmarekani huyo mwenye asili ya Afrika, mchana kweupe mbele ya kadamnasi ya watu, huku muhanga wa ukatili huo akilalamika hawezi kupumua hadi alipokata roho.
Muda mchache kabla ya kukata roho, George Floyd mbali na kusikika akilalamika hawezi kupumua, alisikika pia akiomba maji na kumbembeleza mzungu huyo katili asimuue, lakini yote hayakusaidia kitu na sasa hivi muuaji huyo ameachiliwa huru.
Jinai ya afisa huyo mzungu imezusha hasira dunia nzima na katika kona zote za Marekani. Hata hivyo, rais wa nchi hiyo, Donald Trump ametoa amri ya kukandamizwa waandamanaji.
Maelefu ya waandamanaji wamejeruhiwa katika maandamano ya wiki za hivi karibuni nchini Marekani.