Sisitizo la Venezuela la kuimarisha uhusiano wa kistratijia na Iran
(last modified Fri, 27 Nov 2020 02:27:25 GMT )
Nov 27, 2020 02:27 UTC
  • Sisitizo la Venezuela la kuimarisha uhusiano wa kistratijia na Iran

Katika miezi michache iliyopita ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Venezuela umekuwa ukiimarika katika nyanja tofauti.

Katika uwanja huo, Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela ameashiria nyanja nyingi za ushirikiano wa Tehran na Caracas na kutaka kuwepo uhusiano wa kistratijia baina ya pande mbili.

Kwa kutilia maanani maendeleo ya pande mbili, Jorge Arreaza amesema nchi mbili hizi ni nguvu kubwa katika maneo yao ambapo licha ya kuwepo masafa marefu ya kijiografia baina yazo, lakini bado zina nyanja nyingi za kuimarisha ushirikiano kuliko inavyodhaniwa na wengi.

Katika maiaka ya karibuni Venezuela imekuwa ikipitia mashinikizo na vitisho vikali kutoka kwa Marekani ambapo watawala wa nchi hiyo wangali wanatoa mashinikizo makali ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya Caracas ili kuitoa madarakani serikali halali ya mrengo wa kushoto inayoongozwa na Rais Nicolas Maduro na kuweka mahala pake serikali nyingine inayolinda na kudhamini maslahi ya Washington. Hii ni katika hali ambayo Maduro ambaye anapendwa sana na wananchi na kuungwa mkono na jeshi la taifa amefanikiwa pakubwa kuzima njama hizo za Marekani na kurejesha hali ya utulivu nchini.

Moja ya meli za mafuta za Iran ikielekea Venezuela licha ya vitisho vya Marekani

Kwa kutekeleza siasa tofauti zinazofaa na pia kwa msaada wa washirika wake, ameweza vile vilekuboresha hali ya uchumi wa nchi hiyo. Katika uwanja huo Venezuela imeomba kupewa msaada na uzoefu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo nayo iko chini ya mashikizo na vikwazo vikali vya Marekani, katika kudhibiti na kukabiliana na migogori ya maadui.

Kwa muda mrefu watawala wa Marekani wamekuwa wakitumia vikwazo kama chombo kizuri cha kutoa mashinikizo dhidi ya mataifa mengine yanayojitawala na hasa Iran. Wamejaribu kutumia mbinu hiyo kuipigisha magoti Iran lakini bila mafanikio yoyote. Mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi ya Marekani si tu kwamba yameshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa dhidi ya Iran bali yameipelekea kuwa na uwezo mkubwa wa ndani na kuifanya ijitegemea katika mambo mengi.

Katika hali hiyo, uhusiano na ushirikiano wa Iran na Venezuela umekuwa ikiimarika katika nyanja tofauti na hasa za kiuchumi. Matunda ya uhusiano huo yameonekana wazi katika miezi ya karibuni ambapo Iran ilituma meli zaek za mafuta kwenda kuisadia Venezuela ambayo ilikuwa inakabiliwa na hali ngumu ya uhaba mkubwa wa nishati kutokana na mashinikizo ya Marekani. Licha ya kuwepo vitisho vya Marekai vya kuzishambulia meli hizo lakini Iran haikutishika bali ilituma meli hizo Venezuela na hivyo kupunguza kwa kiasi fulani matatizo ya nishati iliyokuwanayo nchi hiyo ya Amereka ya Latini.

Katika upande wa pili na licha ya kuwepo vitisho vya Marekani na washirika wake, Iran miezi kadhaa iliyopita ilifungua duka kubwa la bidhaa katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas kwa jila la Megasis. Jambo hilo liliwakasirisha sana viongozi wa Marekani ambapo mmoja wa wabunge wa nchi hiyo alimwandikia barua Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje, akielezea wasiwasi wake na kumuonya juu ya kuimarika uhusiano wa Iran na Venezuela. Wasi wasi huo umebainishwa katika hali ambayo viongozi wa Caracas na Tehran wanasisitiza udharura wa kuimarishwa zaidi ushirikiano wa pande mbili katika nyanja tofauti.

Duka kubwa la bidhaa za Iran lililofunguliwa mjini Caracas licha ya vikwazo vya Marekani

Carlos Ron, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela huku akisistiza kwamba Venezuela kuwa na uhusiano wa kibiashara na Iran au nchi nyingine yoyote ile ni haki ya nchi hiyo inayofuatiliwa kisheria amesema, suala linalopasa kutazamwa kwa wasi wasi mkubwa na jamii ya kimataifa ni hatua ya serikali ya Marekani ya kupuuza na kukanyaga sheria za kimataifa na hasa mfumo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa kutilia maanani vikwazo vikali vinavyotekelezwa na Marekani dhidi ya nchi mbili za Iran na Venezuela, ni wazi kuwa kuimarishwa ushirikiano baina ya nchi mbili hizi ni jambo la kawaida kabisa na ambalo linatekelezwa kwa ajili ya kutatua matatizo na kudhamini maslahi ya watu wa nchi mbili. Wakati huo huo hiyo ni dalili ya wazi inayothibitisha kwamba vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi hizo vimegonga mwamba.

Tags