Wabunge 150 wa Marekani wamtaka Biden airejeshe nchi hiyo katika JCPOA
Wabunge 150 wa chama cha Democratic nchini Marekani wamemuandikia barua rais mteule wa nchi hiyo, Joe Biden wakiunga mkono azma yake ya kutaka kuirejeshe nchi hiyo kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA pasi na masharti yoyote mapya.
Kusainiwa kwa waraka huo na wabunge 150 wa chama tawala kunamaanisha kuwa, ni muhali kwa chama cha Republican cha Donald Trump kuchukua hatua yoyote ya kuzuia utekelezaji wa mpango huo wa kuirejesha Marekani katika mapatano hayo ya kimataifa.
Wabunge 34 pekee ndio hawajasaini waraka huo wa kuunga mkono azma hiyo ya Biden ya kutaka kuirejeshe nchi hiyo kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Trump mwezi Mei mwaka 2018 alichukua hatua ya upande mmoja ya kuiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya nyuklia, na kurejesha vikwazo shadidi dhidi ya Iran.
Kitendo hicho cha kukanyaga mapatano ya kimataifa yenye baraka za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimeendelea kukosolewa ndani na nje ya nchi hiyo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa, ikiwa itaondolewa vikwazo na Marekani, kisha nchi hiyo ikarudi tena kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, nayo pia itatekeleza kikamilifu ahadi na majukumu yake kuhusiana na makubaliano hayo.