Mwangwi wa kubwagwa Trump, wapinzani wa Venezuela wapata pigo jipya
(last modified Fri, 08 Jan 2021 07:04:16 GMT )
Jan 08, 2021 07:04 UTC
  • Kibaraka mkubwa wa Marekani,  Juan Guaidó,
    Kibaraka mkubwa wa Marekani, Juan Guaidó,

Baada ya Donald Trump kubwagwa katika uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020 huko Marekani, sasa wafuasi, mashabiki na vibaraka wake wa nje, nao wameanza kuonja makali ya kuwa vibaraka wa Marekani.

Tukio la karibuni kabisa ni uamuzi wa Umoja wa Ulaya na kundi la nchi za Lima wa kutambua rasmi matokeo ya uchaguzi wa bunge nchini Venezuela na kuacha kuwaunga mkono wapinzani wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Uingereza la Financial Times, Josep Borrell, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Jumatano alitangaza kwamba Brussels inayatambua matokeo ya uchaguzi wa Bunge la Venezuela na haimtambui Juan Guaidó, kibaraka wa Marekani ambaye wakati wa urais wa Donald Trump alijitangaza kinyume cha sheria kuwa rais wa Venezuela, na Trump akamtambua rasmi.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

 

Mbali na Umoja wa Ulaya, kundi la Lima linaloundwa na nchi 12 za Amerika ya Latini nalo limetoa taarifa rasmi na kutangaza kuwa linayatambua matokeo ya uchaguzi wa bunge la Veneuela. Taarifa ya nchi hizo hata haikutaja kabisa suala la kumtambua Juan Guaidó.

Baraza la Taifa la Venezuela lilichaguliwa mwezi Disemba 2020 na lilianza kufanya kazi rasmi siku ya Jumanne ya tarehe 5 Januari 2021.

Siku hiyo hiyo ya Jumanne, baraza hilo lilimfukuza Juan Guaidó katika uspika wa bunge na kumchagua Luis Eduardo Parra Rivero ambaye ni mfuasi wa chama tawala, kuwa spika mpya.

Karibu miaka miwili nyuma, Guaidó alijitangaza kuwa rais wa Venezuela kwa kuchochewa na serikali ya Donald Trump ya Marekani. Hata hivyo wafuasi wake walishindwa vibaya katika uchaguzi wa bunge wa Jumapili wiki hii huko Venezuela.

Tags