Italia pia yasitisha mauzo ya silaha kwa Saudia na Imarati
(last modified Sat, 30 Jan 2021 07:52:35 GMT )
Jan 30, 2021 07:52 UTC
  • Italia pia yasitisha mauzo ya silaha kwa Saudia na Imarati

Serikali ya Italia imesimamisha uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, baada ya wanaharakati na wabunge wa nchi hiyo ya Ulaya kuonya kuwa, silaha hizo zinatumika kukanyaga haki za binadamu nchini Yemen.

Katika taarifa jana Ijumaa, Luigi Di Maio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia alisema, "hii ni hatua tuliyoafikia kuwa ya dharura na ujumbe wa wazi kutoka nchi hii. Kwetu sisi, kuheshimu haki za binadamu ni wajibu usiovunjika."

Harakati za kupinga mauzo ya silaha kwa Saudia na Imarati chini ya mwavuli wa Italian Peace and Disarmament Network zimepongeza hatua hiyo na kusisitiza kuwa, kitendo hicho kwa uchache kitazuia uuzaji wa mabomu 12,700.

Mwaka 2018, Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte aliahidi kuwa nchi hiyo itasitisha mauzo ya silaha kwa Saudia, kufuatia mauaji ya kikatili ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal-Saud.

 Luigi Di Maio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia

Mapema wiki hii, serikali ya Joe Biden ilitagaza kusitisha uuzaji silaha za Marekani kwa Saudia na ndege za kivita aina ya F-35 kwa Imarati. Siku chache kabla ya Biden kuapishwa kuwa rais mpya wa Marekani, Donald Trump, rais wa nchi hiyo aliyemaliza muda wake aliafiki mpango wa kuiuzia Imarati ndege 50 za kivita aina ya F35 zenye thamani ya dola bilioni 23.

Vita vya kidhulma vya Saudia na waitifaki wake huko Yemen tokea Machi 2015 hadi sasa vimesababisha kuuliwa Wayemeni zaidi ya elfu 16, kujeruhiwa makumi ya maelfu na kuwa wakimbizi mamilioni ya wengine. 

Tags