Blinken na madai mapya kwa ajili ya kurejea katika JCPOA
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwa mara nyingine tena amekariri hamu ya Washington ya kutaka kurejea katika mapatano ya JCPOA na kisha akatoa madai mapya kama sharti la kurejea katika mapatano hayo.
Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya NBC, Antony Blinken amekariri kuwa, nchi yake ina hamu ya kurejea katika ahadi yake ya huko nyuma kuhusu mapatano hayo na bila ya kuashiria namna serikali ya Marekani yenyewe ilivyojitoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo mwaka 2018 amesema: iwapo Iran itarejea katika majukumu yake ndani ya mapatano ya JCPOA Marekani pia ina hamu ya kutekeleza jambo hilo.
Akiendelea na madai yake Blinken ameongeza kuwa: hivi sasa Iran inahitaji miezi kadhaa mingine ili kumiliki mada zinazohitajika kwa ajili ya kuunda silaha za nyuklia.
Blinken ametoa madai hayo katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha mara kadhaa kuhusu kuwa na lengo la kuunda silaha za nyuklia na kusisitiza kuwa, miradi yake ya nyuklia ni kwa ajili ya malengo ya amani. Aidha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) imesisitiza kuwa miradi ya nyuklia ya Iran ni ya malengo ya amani.