Umoja wa Mataifa: Hali ya Myanmar inatia wasiwasi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i66886-umoja_wa_mataifa_hali_ya_myanmar_inatia_wasiwasi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa hali ya Myanmar inatia wasiwasi na amemtaka mjumbe wake maalumu nchini humo kutayarisha ripoti kuhusu hali ya sasa ya Myanmar.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 15, 2021 12:11 UTC
  • Antonio Guterres
    Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa hali ya Myanmar inatia wasiwasi na amemtaka mjumbe wake maalumu nchini humo kutayarisha ripoti kuhusu hali ya sasa ya Myanmar.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric imesema kuwa, Antonio Guterres ana wasiwasii mkubwa kuhusu hali ya Myanmar ikiwa ni pamoja na kuongezeka utumiaji wa mabavu na vilevile ripoti za kutumwa magari ya kijeshi katika aghlabu ya miji.

Stéphane Dujarric amesema kuendelea utumiaji wa mabavu, kueneza woga na mateso yanayofanywa na maafisa wa usalama havikubaliki na kuongeza kuwa, Katibu Mkuu wa UN Antonio Guttes amelitaka jeshi na polisi ya Myanmar kudhamini haki ya mikusanyiko ya amani na kutowakandamiza waandamanaji.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa: Kuendelea kukamatwa wanasiasa, viongozi wa serikali, wanaharakati wa jumuiya za kiraia, wadau wa vyombo vya habari na vilevile kubanwa huduma za intaneti na huduma nyinginezo nchini Myanmar ni mambo yanayotia wasiwasi.

Waandamanaji nchini Myanmar

Stéphane Dujarric amesema kuwa Umoja wa Mataifa utaeendelea kutetea utawala wa sheria, haki za kidemokrasia na haki za binadamu za watu wa Myanmar. Amesema Katibu Mkuu wa UN amewataka viongozi wa jeshi la Myanmar wamruhusu mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kutembelea nchi hiyo na kutayarisha ripoti kuhusu hali inayotawala Myanmar. 

Tarehe Mosi mwezi huu wa Februari jeshi la Myanmar lilidhibiti madaraka ya nchi baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.