Feb 18, 2021 07:08 UTC
  • Sergey Lavrov
    Sergey Lavrov

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia imetangaza kuwa misimamo ya maafisa wa nchi za Magharibi kuhusiana na takwa la kuachiwa huru mpinzani wa serikali ya Moscow anayeshikiwa na vyombo vya dola ni kielelezo cha uingiliaji kati katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia imesema kuwa, takwa la Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya la kuachiwa huru mpinzani wa serikali ya Moscow, Alexei Navalny, ni uingiliaji kati katika masuala ya ndani unaolaaniwa na Russia.

Wakati huo huo maafisa wa serikali ya Moscow wanasisitiza kuwa ukosoaji wa nchi za Ulaya na Marekani dhidi ya kutiwa nguvuni Alexei Navalny hauna mashiko yoyote ya kisheria.

Alexei Navalny

Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrel, amesema kuwa kuna uwezekano wa kuiwekea vikwazo Russia. Borrel ameyasema hayo baada ya kushadidi hitilafu na mzozo wa kidiplomasia baina ya Russia na nchi za Ulaya na baada ya Moscow kuwatimua wanadiplomasia kadhaa wa nchi za Magharibi kutokana na kushiriki katika maandamano haramu ya kumuunga mkono Alexei Navalny mjini Moscow. 

Mpinzani huyo wa serikali ya Russia amekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma kadhaa ikiwa ni pamoja na kushirikiana na shirika la ujasusi la Marekani CIA. 

Tags