Kukiri Obama kuwepo ubaguzi na tofauti za kitabaka nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i6718-kukiri_obama_kuwepo_ubaguzi_na_tofauti_za_kitabaka_nchini_marekani
Rais Barack Obama wa Marekani amekiri kuwa kungali kuna ubaguzi wa rangi na tofauti za kitabaka ndani ya jamii ya nchi hiyo na kutaka zichukuliwe hatua muhimu kukabiliana na suala hilo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 09, 2016 07:58 UTC
  • Kukiri Obama kuwepo ubaguzi na tofauti za kitabaka nchini Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani amekiri kuwa kungali kuna ubaguzi wa rangi na tofauti za kitabaka ndani ya jamii ya nchi hiyo na kutaka zichukuliwe hatua muhimu kukabiliana na suala hilo.

Obama aliyasema hayo siku ya Jumamosi katika mahafali ya kuhitimu masomo wanachuo wa Chuo Kikuu cha Howard mjini Washington.

Kwa mujibu wa Obama, Marekani ina ufa wa kitabaka katika fursa za kiuchumi. Kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Marekani ni takribani asilimia tano, lakini kiwango hicho kwa Wamarekani wenye asili ya Afrika kinafikia asilimia saba. Kwa mujibu wa Barack Obama, idadi ya wafungwa nchini Marekani ni karibu milioni mbili na laki mbili, ambao ni wengi mno kulinganisha na laki tano waliokuwepo mwaka 1983. Rais wa Marekani amesema, raia weusi wanaofungwa jela idadi yao ni mara sita zaidi kulinganisha na wenzao wazungu; hivyo ameitaka Kongresi ipitishe mipango ya kufanyia marekebisho sheria za makosa ya jinai.

Ni mara kadhaa sasa Obama, akiwa rais pekee mweusi katika historia ya Marekani, amekuwa akithibitsiha kuwepo ubaguzi wa rangi nchini humo na kusisitizia ulazima wa kupambana na tatizo hilo. Mwezi Juni mwaka jana pia aliashiria vitendo mbalimbali vya ubaguzi na ukatili wanaofanyiwa raia weusi na kubainisha kwamba licha ya kuboreka mitazamo juu ya uwepo wa watu wa asili na rangi tofauti nchini Marekani, lakini wingu zito la enzi za utumwa lingali limetanda kwenye anga ya jamii ya nchi hiyo, na urithi huo ungali ni sehemu ya Vinasaba (DNA) vya Wamarekani.

Licha ya madai ya utiaji chumvi ya kuheshimiwa uhuru wa mtu binafsi na haki za binadamu nchini Marekani lakini hali ya Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao idadi yao haipungui watu milioni 45 si ya kuridhisha kutokana na kukabiliwa na anuai za ubaguzi wa siri na wa dhahiri. Rangi na asili ya mtu ina nafasi muhimu katika kuamua nani apige hatua mbele na nani abaki nyuma kiustawi nchini Marekani. Pamoja na raia weusi kuunda asilimia 14 ya idadi ya watu wote nchini Marekani lakini hawajanufaika kama inavyostahiki na utajiri na huduma za elimu na za ustawi wa jamii nchini humo wakiwa ndio wanaokumbwa zaidi na masaibu na matatizo katika jamii. Ingawa kulikuwa na matarajio kwamba kwa kuchaguliwa Barack Obama, akiwa rais wa kwanza mweusi nchini Marekani, hali za raia wenye asili ya Kiafrika zitaboreka lakini kinachoshuhudiwa ni kuendelea kuwa mbaya hali zao kiuchumi na kijamii.

Umoja wa Mataifa umekuwa kila mara ukiitaka Marekani ichukue hatua za kupambana na ubaguzi wa rangi ndani ya jamii ya nchi hiyo na hata kuwaonya viongozi wa White House kuwa hatua za serikali hiyo na polisi ya nchi hiyo kuhusiana na raia wenye weusi zinakinzana na Tangazo la Haki za Binadamu la umoja huo.

Katika hotuba yake ya Jumamosi, Barack Obama aliashiria nukta muhimu kadhaa kuhusu ubaguzi dhidi ya Wamarekani weusi. Miongoni mwao ni kuwepo ubaguzi na upendeleo wa wazi baina ya wazungu na watu weusi katika suala la ajira. Hata kama watakuwa na sifa zinazotakiwa za kielimu na kitaalamu, Wamarekani wenye asili ya Afrika wana bahati ndogo zaidi ya kupata ajira kulinganisha na wenzao wazungu. Idadi ya raia hao wanaotumikia vifungo jela ni kubwa, na suala hilo lina uhusiano wa moja kwa moja na uhaba wa suhula na umasikini mkubwa unaoshuhudiwa miongoni mwa Wamarekani weusi ambao unazidisha uwezekano wa wao kujihusisha na vitendo mbalimbali vya uhalifu.../