Biden akosolewa kwa kutomuwekea vikwazo Bin Salman kwa mauaji ya Khashoggi
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekosoa vikali hatua ya utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani ya kuamua kutomuwekea vikwazo Mohammad Bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, licha ya kukiri katika ripoti kuwa ndiye aliyetoa amri ya kuuawa Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari aliyekuwa akiukosoa utawala wa Aal-Saud.
Agnes Callamard, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia jinai za mauaji ameitaka Marekani imuwajibishe Bin Salman kwa kumwekea vikwazo iwapo inataka kutenda haki na uadilifu kwa dhati kuhusiana na mauaji hayo ya kikatili.
Kwa upande wake, Andrea Prasow, Naibu Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch mjini Washington amesema hatua ya kushindwa kumuwekea vikwazo Bin Salman haina mantiki wala busara.
Amesema, "nukta kwamba Marekani imewawekea vikwazo washirika wengi wa Muhammad Bin Salman lakini si yeye binafsi, inatuma ujumbe mbaya sana kwamba, kadiri unavyokuwa katika ngazi za juu serikalini, ndivyo unavyoweza kufanya jinai na ukose kuwajibishwa."
Naye Seth Binder, afisa wa shirika la kiraia la Project on Middle East Democracy (POMED) amenukuliwa na tovuti ya habari ya Middle East Eye akisema kuwa, iwapo suala la haki za binadamu ndio msingi wa sera za nje za Marekani kama inavyodai serikali ya Biden, basi ni kichekesho kuwavua lawama makatili mithili ya Bin Salman.
Taasisi ya Taifa ya Taarifa za Kijasusi za Marekani ilisema katika ripoti jana Ijumaa kuwa, Mohammad Bin Salman alibariki kutekwa nyara na kuuliwa Jamal Khashoggi katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki mwaka 2018. Baada ya kusambaza ripoti hiyo, Marekani imewawekea vikwazo vya viza maafisa 76 wa Saudi Arabia.
Mwakilishi wa Marekani, Adam Schiff ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Intelijensia ya Bunge la nchi hiyo amepongeza hatua ya serikali ya Biden ya kuanika ripoti hiyo, lakini anasisitiza kuwa, Washington ilitakiwa iende mbali zaidi na kumbebesha dhima Bin Salman.