Makundi 32 ya Marekani yamtaka Biden airejesha nchi hiyo katika JCPOA
Makundi 32 ya Marekani yamemtaka Rais wa nchi hiyo Joe Biden airejesha Washington katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA haraka iwezekanavyo.
Gazeti la The Hill liliripoti hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, makundi hayo ya kiraia yametoa mwito huo katika barua yao yaliyoiandikia Ikulu ya White House ya Marekani.
Katika barua hiyo, makundi hayo yamesema pendekezo la Biden kwamba Iran inapaswa kupunguza kiwango cha urutubishaji urani kabla ya Marekani kurejea katika mapatano hayo yumkini likakwamisha au kuweka kizingiti katika mazungumzo ya kuyanusuru mapatano hayo ya kimataifa.
Barua hiyo imeeleza bayana kuwa, Marekani ndiyo iliyokiuka wa kwanza makubaliano hayo ya JCPOA na kwamba haingii akilini kwa mkiukaji wa mapatano kutoa masharti.
Makundi hayo yamemtaka Rais Biden atekeleza ahadi yake ya kutofuata mkumbo wa mtangulizi wake Donald Trump katika utekeleza wa sera za nje za nchi hiyo.
Barua hiyo imemkumbusha Rais wa Marekani juu ya matamshi yake mwenyewe ya mwaka jana, alipokariri mara kadhaa kuwa sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu iliyokuwa ikitekelezwa na utawala wa Trump dhidi ya Iran imefeli na kugonga mwamba.
Makundi hayo 32 ya Marekani yamesisitiza katika barua yao kwa Biden kuwa, kadri chembe chembe za 'mashinikizo ya juu kabisa' zinaendelea kuwepo, ndivyo suluhu ya kidiplomasia baina ya Tehran na Washington inazidi kuwa ngumu.