Bernie Sanders: Umasikini baina ya watoto umeongezeka nchini Marekani
Seneta wa jimbo la Vermont nchini Marekani amesema kuwa, kiwango cha umasikini baina ya watoto nchini humo kimeongezeka mno na kufikia kiwango cha juu kabisa ikilinganishwa na mataifa muhimu duniani.
Bernie Sanders amesema katika ujumbe wake aliouandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter na kukosoa vikali sera zisizo sahihi za kiuchumi katika nchi hiyo.
Seneta huyo amesema wazi kuwa, sera za kiuchumi nchini Marekani zimekuwa zikiifanya jamii ndogo ya nchi hiyo kuzidi kuwa matajiri na wakati huo huo, ikikung'uta mifuko ya vibarua ambao ni wa tabaka la nchini katika jamii.
Hivi karibuni ilitolewa ripoti pia inayoonyesha kuwa, kusambaa virusi vya Corona nchini Marekani na mazingira yaliyosababishwa na utendaji mbovu wa serikali iliyopita ya Trump ni mambo ambayo yamepelekea kuongezeka matatizo ya kijami na kiuchumi yanayoikabili nchi hiyo.
Katika miezi ya karibuni mamilioni ya wafanyakazi nchini humo wamepoteza ajira zao na sasa Wamarekani zaidi ya milioni 29 hawana chakula cha kutosha. Bernie Sanders ameongeza kuwa, watu milioni 40 pia wanakabiliwa na hatari ya kupoteza makazi yao.
Uchumi wa Marekani umeathirika vibaya sana tangu janga la corona liikumbe nchi hiyo. Hadi sasa maelfu ya makampuni na viwanda vya uzalishaji vimefungwa huko Marekani tangu nchi hiyo ikumbwe na maambukizi ya corona.