'Kufungiwa akaunti ya Twitter kumemuumiza zaidi Trump kuliko kushindwa katika uchaguzi'
Mpwa wa rais wa zamani wa Marekani amesema, kufungiwa Donald Trump akaunti yake ya Twitter na kunyimwa fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya gofu vimemuumiza zaidi kuliko pigo alilopata kwa kushindwa katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.
Mary Trump ameliambia gazeti la Daily Mail linalochapishwa nchini Uingereza kuwa, huenda kufungiwa Trump akaunti yake ya twitter na kunyimwa fursa ya kuendesha mashindano ya mchezo wa gofu ya mwaka 2022, yakawa ndio matukio machungu zaidi katika kipindi cha miaka minne ya urais wake.
Mary Trump ameongeza kuwa, bila ya twitter, rais huyo wa zamani wa Marekani hana uwezo wa kuwavutia watu na raia wa Marekani.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano yake na gazeti hilo la Uingereza, mpwa huyo wa rais wa zamani wa Marekani amesema haliangalii kwa jicho zuri suala la Trump kugombea tena urais katika uchaguzi wa mwaka 2024 na kueleza kwamba, hiyo ni mbinu yake nyingine ya kutaka kuwahadaa wafuasi wake ili aweze kujipatia fedha.
Mnamo Januari 8, 2021, mtandao wa kijamii wa Twitter uliifunga moja kwa moja akaunti ya twitter ya Trump baada ya wafuasi wake kuvamia jengo la bunge la Marekani.
Aidha Shirika la Gofu la Marekani limekata mawasiliano yake na klabu ya gofu ya Donald Trump iliyoko katika mji wa Badminster jimboni New Jersey na kughairisha mashindano ya mwaka 2022 ya mchezo huo yaliyokuwa yafanyike katika viwanja vya gofu vya rais huyo wa zamani wa Marekani.../