Mar 19, 2021 02:35 UTC
  • Russia: Marekani inapasa kuomba radhi kwa kumtukana Putin

Naibu Mkuu wa Baraza la Shirikisho (Bunge la Seneti la Russia) ametangaza kuwa, Marekani inapaswa kuomba radhi kwa hatua yake ya kumtukana Rais Vladimir Putin wa Russia.

Konstantin Kosachev jana Alkhamisi aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: hatua ya kumuita Moscow Anatoly Antonov Balozi wa Russia mjini Washington ni jibu sahihi kwa matamshi ya Rais Joe Biden wa Marekani. 

Kosachev ameongeza kuwa, matamshi kama hayo hayakubaliki kivyovyote vile; na yanavuruga zaidi uhusiano wa pande mbili. Naibu Mkuu wa Baraza la Shirikisho (Bunge la Seneti la Russia) amebainisha kuwa, kitendo cha kumuita nyumbani Balozi wa Russia mjini Washington haitakuwa radiamali ya mwisho ya Kremlin kwa matamshi ya Biden iwapo Marekani haitaomba radhi.  

Rais Putin wa Russia 

Idara ya Intelijinsia ya Marekani Jumanne wiki hii ilitoa ripoti ya siri kuhusu kile kilichotajwa kuwa ni kuingiliwa uchaguzi wa mwaka 2020 wa Marekani ambayo ilieleza kuwa Putin alisimamia njama kubwa za kumchafulia Joe Biden nafasi yake ya kugombea kiti cha urais.  Aidha katika mahojiano yake na televisheni ya ABC News, Rais Joe Biden wa Marekani alisema kuwa, alimtahadharisha Rais Putin kuhusu suala hilo katika mazungumzo ya simu aliyofanya naye mwezi Januari. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa imemuita nyumbani balozi wake huko Washington kufuatia matamshi hayo yaliyotolewa na Joe Biden ambaye amemtaja Rais Putin wa Russia kuwa ni muuaji na kumtuhumu kuingilila masuala ya uchaguzi wa nchi yake huku Marekani ikisema kuwa Moscow inapasa kufidia hatua yake hiyo. 

Tags