Vitendo vya uhalifu vyaongezeka kwa asilimia 25 nchini Marekani
Polisi ya Federali ya Marekani FBI imetangaza habari ya kuongezeka kwa asilimia 25 vitendo vya uhalifu na jinai nchini humo katika mwaka uliopita wa 2020.
Televisheni ya CNN ya Marekani imetangaza habari hiyo na kuongeza kwamba, ijapokuwa majumuisho ya mwisho ya ripoti hiyo yatatolewa rasmi mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu wa 2021 lakini takwimu za awali zinaonesha kuwa, kuna ongezeko lisilopungua la asilimia 25 la vitendo vya uhalifu nchini Marekani na kiwango hicho cha jinai na uhalifu uliotokea nchini humo mwaka jana 2020 hakijawahi kushuhudiwa tangu mwaka 1995.
Kwa mujibu wa ripoti za FBI zilizotangazwa na televisheni ya CNN huko Marekani, katika kipindi cha miezi mitatu ya awali ya mwaka huu wa 2021 idadi ya vitendo vya uhalifu nchini humo vimeongezeka kwa asilimia 18 ikilinganishwa na muda kama huu mwaka uliopita. Takwimu hizo ni matokeo ya uchunguzi uliofanyika katika miji 37 ya Marekani.
Kwa upande wake televisheni ya Fox News ya Marekani pia imeripoti kuwa, vitendo vya mauaji ya watu katika mji wa Portland wa jimbo la Oregon Marekani vimeongezeka kwa asilimia 2,000. Vitendo vya uhalifu, mashambulizi, utekaji nyara na utumiaji mbaya wa silaha umeongezeka pia katika kona mbalimbali za Marekani.
Maelfu ya watu wanauawa na kujeruhiwa kwa risasi kila mwaka katika maeneo tofauti ya Marekani. Ripoti rasmi za serikali za nchi hiyo zinaonesha kuwa silaha zinazomilikiwa na raia nchini Marekani ni baina ya milioni 270 hadi milioni 300, yaani kila raia wa Marekani kwa uchache anamiliki silaha moja ya moto.