Mar 22, 2021 11:09 UTC
  • Russia: Kujiondoa Marekani JCPOA kunaonesha haiwezi kutekeleza mapatano

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kitendo cha Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayofahamika kwa kifupi kama JCPOA kinaashiria namna Washington haiwezi kuheshimu wala kutekeleza mapatano na mikataba ya kimataifa inayoyafunga.

Sergei Lavrov amesema hayo leo Jumatatu katika kikao na waandishi wa habari baada ya kuwasili nchini China kwa ziara rasmi ya kikazi.

Lavrov ameongeza kuwa, Marekani si tu ilijiondoa kwenye makubaliano hayo ya nyuklia, lakini pia inazuia washiriki wengine wa mapatano hayo ya kimataifa kufungamana nayo kama ilivyoashiriwa kwenye Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amebainisha kuwa, hatua hiyo ya upande mmoja ya Washington kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 ni ukanyagaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Trump alipoiondoa US katika JCPOA

Ikumbukwe kuwa, utawala uliopita wa Donald Trump nchini Marekani uliiondoa nchi hiyo kwenye makubaliano ya JCPOA mnamo Mei mwaka 2018, na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran chini ya kaulimbiu ya 'mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi.'

Kadhalika utawala wa sasa wa Joe Biden haujachukua hatua yoyote ya maana ya kuirejesha Marekani katika mapatano hayo ya kimataifa yenye baraka kamili za Baraza la Usalama la UN.

Tags