Marekani yaibua shaka kuhusu kufungamana kwake na JCPOA na kuondoa vikwazo
Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika serikali ya Marekani alisema Alkhamisi kwamba hakuna dhamani ya kimaandishi itakayotolewa na serikali hiyo kuthibitisha kwamba haitajiondoa tena katika mapatano ya nyukilia na Iran na madola mengine makuu ya dunia, mashuhuri kama JCPOA.
Afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kwamba iwapo serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani itafikia maelewano na Iran pamoja na nchi nyingine wanachama wa kundi la 1+4 na kuamua kurejea katika mapatano ya JCPOA basi suala hilo litakuwa limefanyika kwa msingi wa nia njema tu na kuwa haitajitoa tena katika mapatano hayo bila sababu muhimu, lakini akaongeza kwamba hakuna dhamana yoyote ya kimaandishi itakayotolewa na serikali ya Washington kuhusu suala hilo.
Kuachwa mwanya wa Marekani kujitoa tena katika mapatano ya JCPOA bila shaka kunathibitisha wazi tabia ya nchi hiyo ya kutoheshimu mikataba ya kimataifa. Serikali ya Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani ilipuuza na kukanyaga wazi wazi ahadi zake za mapatano ya JCPOA yaliyopitishwa kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hatimaye kuamua kujitoa katika mapatano hayo mwezi Mei 2018. Baada ya kuonyesha kiburi hicho mbele ya jamii ya kimataifa, iliamua kuiwekea Iran vikwazo vikali chini ya siasa zake za 'mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Tehran' ili kuipigisha magoti na kuilazimisha ukubaliane na matakwa yake yaliyo kinyume cha sheria. Licha ya kutekeleza siasa hizo za mabavu dhidi ya Tehran lakini serikali ya Trump mwenyewe ilikiri hadharani kushindwa kuilazimisha Iran ifuate matakwa yake ya kibabe.
Hivi sasa serikali ya Joe Biden imekuwa ikidai kwamba inataka kurejea kwenye mapatano hayo ya kimataifa na kutaka kufanya mazungumzo ya pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uwanja huo. Pamoja na hayo inasisitiza kwamba hata kama itarudi kwenye mapatano hayo lakini haitatoa dhamana yoyote ya maandishi ya kuthibitisha kuwa haitajitoa tena kwenye mapatano hayo bila kuwepo sababu yoyote ya kimsingi. Kwa ibara nyingine ni kuwa hata kama Marekani itareja kwenye mapatano ya JCPOA lakini bado kutaendelea kuwepo shaka ya nchi hiyo kutekeleza majukumu na ahadi zake.
Madai ya serikali ya Biden kutaka kurudi katika mapatano ya JCPOA yameyafanya mapatano hayo yachukue sura ya kufungamana na uamuzi wa serikali tofauti zinazokuja madarakani White House, suala ambalo limethibitishwa kivitendo hadi sasa.
Madai yaliyotolewa na utawala wa Trump katika kujitoa katika mapatano ya JCPOA wakati huo ni kwamba hayakuwa yameidhinishwa na Congress na hivyo hakukuwepo na kuzuizi chochote cha kuizuia serikali kujitoa kwenye mapatano hayo. Wakati huo huo Trump alidai kwamba mapatano hayo hayakudhamini maslahi ya Marekani na kwamba hayakuwa na dhamana za kutosha za kuzuia ustawi wa nyuklia wa Iran.
Suala jingine lililosisitizwa na afisa huyo wa Marekani ni kwamba vikwazo vitakavyojadiliwa kuondolewa ni vile vinavyohusiana na mapatano ya JCPOA tu. Kwa hatua hiyo, kwa hakika serikali ya Biden imegawanya vikwazo dhidi ya Iran katika makundi mawili ya vikwazo vinavyoweza kusimamishwa kwa muda na vile visivyoweza kuondolewa kabisa.
Hayes Brown, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Matekani na mhariri wa jarida la kanali ya televisheni ya MSNBC amekiri kwamba Marekani ndiyo imeyaweka mapatano ya JCPOA katika hali ya kulegalega ya hivi sasa na kuongeza kwamba: Ni jambo la kuchekesha kwa serikali ya Joe Biden kuitaka Iran irejee kwanza katika utekelezaji kamili wa mapatano.
Rob Malley, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran na ambaye anaoongoza ujumbe wa Marekani katika mazungumzo ya Vienna Austria amesema kwamba vikwazo vinavyoweza kuondolewa dhidi ya Iran ni vile tu vinavyokiuka mapatano ya JCPOA na kuwa vingine vyote vinavyohusiana na tuhuma zingine dhidi ya Tehran vitaendelea kutekelezwa. Kwa ufupi ni kwamba serikali ya Biden si tu kuwa haiko tayari kutangaza hadharani kuwa itaheshimu mapatano ya JCPOA bali haiko tayari pia kuondoa vikwazo vya upande mmoja na haramu ambavyo viliwekwa na utawala wa Trump dhidi ya Iran. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa serikali ya Biden inaendeleza siasa zile zile za serikali tangulizi ya Trump dhidi ya Tehran, siasa ambazo hadi sasa zimeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.