May 02, 2021 02:22 UTC

Baada ya kupita siku 100 tokea Rais Joe Biden wa chama cha Democrat achukue madaraka ya Marekani, watu wamekuwa wakitathmini utendaji wa serikali yake katika kipindi hiki, kipindi ambacho baadhi ya wataalamu wanasema kwamba licha ya kufanikiwa katika baadhi ya sehemu lakini ameshindwa pakubwa kutekeleza ahadi alizotoa katika kampeni za uchaguzi.

Inaonekana serikali ya Biden imefanikiwa kwa kiwango fulani katika uwanja wa kupambana na virusi vya corona na pia kuhuisha uchumi wa Marekani. Kwa kutilia maanani kuwa zaidi ya Wamarekani milioni 32 wameathirika na virusi vya corona ambapo zaidi ya laki 5.75 tayari wamepoteza maisha lakini kwa mujibu wa takwimu rasmi,  zaidi ya raia milioni 100 wa nchi hiyo wamepata dozi ya pili ya chanjo ya corona na hivyo kupunguza pakubwa idadi ya watu wanaopoteza maisha kutokana na virusi hivyo.

Katika uhuishaji uchumi, wizara ya biashara ya Marekani imetoa ripoti ikitangaza kukua uchumi wa nchi hiyo kwa asilimia 6.4 katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu wa 2021. Msaada wa kifedha kwa mashirika madogo ya kibiashara na viwanda vikubwa, kutolewa chanjo kwa raia, kuandaliwa mazingira yanayofaa kwa ajili ya watu kurejea makazini na kufunguliwa uchumi ni baadhi ya mambo ambayo inasemekana yamechangia hali hiyo ya kuridhisha kimaendeleo.

Joe Biden

Pamoja na hayo lakini serikali ya Biden imekabiliwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wa baadhi ya ahadi ilizotoa. Moja ya ahadi hizo ni kuhusu suala la wahamiaji ambapo serikali yake imeshindwa kutatua matatizo ya wahamiaji ambapo kwa sasa kuna idadi kubwa ya wahamiaji haramu ambao wamekwama katika mipaka ya nchi hiyo.

Wakosoa wa Biden wanaamini kwamba ahadi alizotoa za kubadilisha siasa za uhamiaji za serikali ya Donald Trump na kuruhusu wahamiaji waingie kirahisi Marekani zimewafanya maelfu ya wahamiaji kutoka nchi za Amerika ya Kati kuamua kuelekea katika mipaka ya kusini mwa nchi hiyo wakitumai kwamba wataruhusiwa kuingia kirahisi nchini humo kwa ajili ya kuanzisha maisha mapya. Hii ni katika hali ambayo taasisi za serikali kuu na za majimbo zimeshindwa kukabiliana na wimbi jipya la wahamiaji.

Hii ni katika hali ambayo mashirika ya kutetea haki za binadamu yanakosoa vikali miamala mibaya wanayofanyiwa wakimbizi na wahamiaji na kusema sehemu wanazowekwa hazifai kabisa kwa maisha ya mwanadamu. Katika radiamali yake kuhusu suala hilo, Biden katika hatuba yake siku ya Ijumaa alikwepa  kwa makusudi kuzungumzia suala hilo na kukataa kulichukulia kuwa mgogoro mkubwa wa wahamiaji. Alisema serikali yake inafanya kila linalowezekana kuwarejesha watoto wahamiaji kwa wazazi wao. Amesema kwamba matatizo ya kiuchumi ambayo yamejitokeza katika mipika ya kusini mwa nchi hiyo yanatokana na uamuzi wa serikali ya mtangulizi wake wa kutoshirikiana na timu ya serikali yake mpya.

Suala jingine ambalo limezidisha mashinikizo dhidi ya serikali ya Biden ni kuongezeka pengo la kijamii ndani ya Marekani na wakati huo huo kudhihiri makundi mawili kinzani ndani ya Congress, ambapo wanachama wa Republican wamekuwa wakipinga wazi wazi na kukataa kupitisha mipango ya kiuchumi na kijamii ya serikali yake.

Biden amewasilisha bungeni mipango ya kupambana na corona, kudhamini bima ya jamii na kuhuisha nafasi za ajira nchini Marekani inayogharibu karibu dola trilioni 6 kwa ajili ya kuhuisha uchumi na miradi ya kijamii nchini humo. Licha ya ahadi alizotia kuhusu athari nzuri za miapngo hiyo, lakini hakuna hatua zozote za kivitendo zinazochukuliwa na maafisa wa White House na wanachama wa chama cha Democrat kwa kuzingatia wingi wao katika Congress na Senate, kwa shabaha ya kuwakinaisha wenzao waunge mkono na kuipigia kura mipango hiyo

Wahamiaji wakiwa kwenye mpaka wa Marekani

Kupuuzwa huko kwa Warepublican kumewapelekea wachukue msimamo wa kupinga mipango yote inayowasilishwa bungeni na serikali ya Biden. Katika hotuba yake ya karibuni kwenye Congress, Biden amewataka wabunge waonyeshe umoja na mshikamano na kuwathibitishia walimwengu kwamba Marekani ina uwezo wa kutatua haraka matatizo yanayoikabili. Wabunge wa chama cha Republican wanasema kuwa ahadi alizotoa Biden za kuimarisha umoja na kuunganisha makundi na vyama vya Marekani chini ya bendera moja ya Marekani, yalikuwa maneno matupu na kwamba tabia na miamala yake inakwenda kinyume na ahadi hizo.

Kwa maneno mengine ni kwamba kinyume na nara alizopiga katika kampeni za uchaguzi yaani za kuiunganisha Marekani na kuifanya kuwa kitu kimoja, rais huyo ameamua kuigawa nchi hiyo katika makundi tofauti hasimu kisiasa na kijamii.

Akifafanua suala hilo,Tim Scott Seneta wa chama cha Republican alisoma ujumbe rasmi wa chama hicho kuhusu hotuba ya Biden katika kikao cha pamoja cha Congress na kusema: Baada ya kupita siku 100 tangu aingie madaraakani, Biden na chama wametutenganisha zaidi.

Tags