FIFA yamteua mwanamke wa Kiislamu kuwa Katibu Mkuu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i7030
Kwa mara ya kwanza katika historia ya kandanda duniani, Shirikisho la Soka Duniani FIFA limemteua mwanamke wa Kiafrika na Muislamu kuwa Katibu Mkuu wa taasisi hiyo ya kimataifa ya kusimamia mpira wa miguu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 14, 2016 06:00 UTC
  • FIFA yamteua mwanamke wa Kiislamu kuwa Katibu Mkuu

Kwa mara ya kwanza katika historia ya kandanda duniani, Shirikisho la Soka Duniani FIFA limemteua mwanamke wa Kiafrika na Muislamu kuwa Katibu Mkuu wa taasisi hiyo ya kimataifa ya kusimamia mpira wa miguu.

Kuteuliwa kwa Fatma Samba Diouf Samoura raia wa Senegal kuwa Katibu Mkuu mpya wa FIFA kumezusha msisimko mkubwa miongoni mwa wadau na wafuatiliaji wa maswala ya soka duniani haswa ikizingatiwa kuwa, wadhifa huo na nyadhifa zingine za juu katika shirikisho hilo zimekuwa zikishikiliwa na wanaume. Kibarua cha kwanza cha mwanamke huyo wa Kiafrika ni kujaribu kulirejeshea hadhi na sura shirikisho hilo ambalo katika miaka ya hivi karibuni limekuwa likikabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Kwa zaidi ya miongo miwili, mwanadiplomasia huyo amekuwa akifanya kazi na idara mbali mbali ya Umoja wa Mataifa.

Tangazo hilo limefanywa na Rais wa FIFA Gianni Infantino katika Kongamano la 66 la FIFA linalofanyika Mexico City, mji mkuu wa Mexico, ikiwa ni kongamano lake la kwanza tangu ateuliwe kuliongoza shirikisiho hilo mwezi Februari mwaka huu, kuja kuchukua nafasi ya Sepp Blatter.

Raia huyo wa Senegal anakuja kurithi mikoba ya Jerome Valcke ambaye alipigwa marufuku kujihusisha na shughuli zozote za soka kwa miaka 12 mapema mwaka huu.

Hii ni mara ya kwanza kwa kongamano la FIFA lililohudhuriwa na viongozi wa Mashirikisho yote duniani ya soka 209 limefanyika nchini Mexico, baada ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986.