Mashirika 130 yataka Canada iache kuhujumu taasisi za Kiislamu
Huku vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vikionekana kushtadi nchini Canada, serikali ya nchi hiyo imekuja na mpango wa kuyafanyia 'ukaguzi' mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Kiislamu nchini humo.
Zaidi ya asasi 130 za kiraia zimeiandikia barua serikali ya nchi hiyo zikiitaka kutazama upya ukaguzi huo wa kibaguzi, unaondeshwa na Mamlaka ya Ushuru Canada (CRA).
Barua ya mashirika hayo ya Kiislamu nchini Canada kama Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada (National Council of Canadian Muslims), Edmonton Islamic Center pamoja na Msikiti wa Jamia wa London jimboni Ontario imetaka serikali ya Ottawa ianzishe uchunguzi kuhusu ukaguzi huo wa kibaguzi unaolenga asasi za Kiislamu pekee.
Sehemu moja ya barua hiyo imesema: Kuzilenga mashirika ya utoaji misaada ya Kiislamu kwa msingi kuwa huenda eti yanafadhili ugaidi, ni chuki dhidi ya Uislamu (Ismalophobia) na mtazamo ghalati dhidi ya jamii ya watu kutokana tu na dini yao.
Haya yanajiri huku Waislamu nchini humo wakiitaka serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua ya kukabiliana na kuzuia vitendo vya chuki, ubaguzi, uhalifu na jinai vinavyotokana na chuki dhidi ya jamii ya Waislamu nchini humo.
Waislamu hao wa Canada hivi sasa wanaishi kwa hofu baada ya kujiri hivi karibuni mauaji ya kutisha dhidi ya familia moja ya Kiislamu katika mji wa London katika jimbo la Ontario nchini humo.
Hii ni katika hali ambayo, taasisi ya uchuguzi wa maoni ya The Angus Reid Institute ilitangaza hivi karibuni kuwa, matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanyika karibuni yameonesha kuwa thuluthi moja ya wananchi wa Canada wanaamini nchi hiyo ina mielekeo ya kibaguzi.