Russia yakanusha kuhusika wakufunzi wake wa kijeshi na mauaji huko CAR
Ikulu ya Russia (Kremlin) imekanusha madai kwamba wakufunzi wa kijeshi wa nchi hiyo waliopo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wamehusika katika mauaji ya raia na kupora mali za watu majumbani.
Marekani, Ufaransa na Uingereza zimewatuhumu wakufunzi wa kijeshi wa Russia kwa kukiuka haki za binadamu na kuwazuia wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yao huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Nchi hizo tatu zimetoa tuhuma hizo dhidi ya Russia katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Alipoulizwa kuhusu ripoti hiyo, Dmitry Peskov Msemaji wa Kremlin amekanusha tuhuma hizo dhidi ya Moscow. Makubaliano ya amani kati ya serikali ya Bangui na makundi 14 ya waasi nchini humo yalisainiwa mwezi Februari mwaka 2019, hata hivyo machafuko na ukosefu wa amani vingali vinaendelea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Itafahamika kuwa, Russia inamuunga mkono Rais wa nchi hiyo Faustin- Archange Touadera ambaye alishinda muhuma wa pili wa urais katika uchaguzi wa Disemba mwaka jana lakini angali anakabiliwa na uasi wa makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha wenye mfungamano na rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Francois Bozize.
Russia imetuma washauri wake wa kijeshi nchini humo kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi hiyo kufuatia mwaliko wa serikali.