Benki ya Dunia yatahadharisha kuhusu ongezeko la madeni ya nchi maskini
Benki ya Dunia imetahadharisha juu ya kuongezeka kwa kiasi kikubwa madeni ya nchi zenye vipato vya chini duniani na taathira zake kwa uchumi wa dunia.
David Malpass Mkuu wa Benki ya Dunia ametaja ongezeko la madeni yanayozikabili nchi maskini duniani kuwa moja ya vitisho vya uchumi wa dunia. Ripoti ya karibuni ya Benki ya Dunia inaonyesha kuwa, madeni ya nchi maskini duniani yameongezeka kwa asilimia 12 na kufikia rekodi ya dola bilioni 860 mwaka 2020.
Amesema ongezeko hilo la madeni ni matokeo ya moja kwa moja ya maambukizi ya virusi vya corona kwa uchumi wa dunia na viongozi wa serikali katika nchi mbalimbali wanapasa kufanya juhudi kupunguza kiwango hicho cha madeni.
Mkuu wa Benki ya Dunia ameongeza kuwa takwimu za madeni kimataifa mwaka 2020 zinaonyesha kuwa kuna ongezeko la hasara na maafa yaliyosababishwa na madeni katika nchi nchi maskini na zile zinazostawi; na nchi zote duniani zinapasa kufanya juhudi ili kuwa na kiwango cha wastani cha madeni kwa kushirikiana pande zote.
Malpass amesisitiza kuwa ipo haja ya kufikia kiwango thabiti cha madeni ili kuzisaidia nchi maskini na kuboresha uchumi na pia kupunguza umaskini duniani.