TICAD inaimarisha vipi nafasi ya Afrika katika siasa na uchumi wa dunia?
Mkutano wa 9 wa Kimataifa wa Maendeleo ya Afrika, Tokyo International Conference on African Development (TICAD), ulimalizika Ijumaa, Agosti 22 kwa kusainiwa mikataba takriban 300 ya ushirikiano kati ya taasisi za Japan na Afrika kuhusu masuala mbalimbali ya afya, teknolojia, elimu, kilimo, maendeleo ya miundombinu na ujenzi wa miundomsingi.
Mkutano wa 9 wa Kimataifa wa Maendeleo ya Afrika, ambao hufanyika kila baada ya miaka 4 kwa lengo la kuendeleza na kutoa kipaumbele kwa nchi za Afrika na kusaidia mchakato wa maendeleo yao, ulifanyika mwaka huu kwa kushirikishwa nchi nyingi za bara hilo. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alisisitiza katika mkutano huo kwamba: 'Afrika lazima iwe na nafasi kubwa katika maamuzi yanayohusu mustakabali wake.' Alisema: 'Kuwa na nafasi kubwa katika kufanya maamuzi ni njia ya Afrika kuimarisha sura na kutetea maslahi yake katika masuala ya kimataifa, hasa katika taasisi za kifedha na kiutawala duniani.'
Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu wa TICAD ilikuwa "Umiliki wa Afrika Kwa Ajili ya Maendeleo Yake Yenyewe na Ushirikiano wa Afrika na Jamii ya kimataifa Kwa Ajili Yake", ambayo ilisisitiza umuhimu wa Afrika kujitegemea na kupewa ushirikiano wa kimataifa.
TICAD imefanyika huku umuhimu wa Bara la Afrika katika nyanja ya siasa na uchumi wa dunia ukidhihirika zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Bara la Afrika lenye idadi ya watu bilioni moja na milioni 200 na maliasili tajiri, ingawa siku zote limekuwa likinyanyaswa na mataifa yenye nguvu duniani, lakini sasa limekuwa uwanja wa ushindani kati ya nchi mbalimbali kwa ajili ya ushawishi wa kiuchumi. Wakati huo huo, kwa kuandaa mkutano wa TICAD, Japan imekuwa ikijaribu kuwa mshirika wa maendeleo wa kutegemewa na Afrika kwa miongo kadhaa sasa.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Afrika ni mojawapo ya vyanzo vikubwa zaidi vya ukuaji duniani, ikiwa na idadi ya watu watakaofikia bilioni 2.5 ifikapo mwaka 2050 na soko la ajira litakalowapokea vijana milioni 450 ifikapo mwaka 2035. Wakati huo huo, ukuaji wa haraka wa miji na mabadiliko ya kidijitali yanaharakisha mabadiliko ya kiuchumi ya bara hilo. Uwekezaji wa kigeni pia unafuata mwelekeo huu huu, kwani kwa mujibu wa ripoti ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo UNCTAD, mtiririko wa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni umefikia zaidi ya dola bilioni 85, jambo ambalo linathibitisha nafasi ya kimkakati ya Afrika katika uchumi wa dunia.

TICAD ya mwaka huu imekuwa muhimu zaidi hasa kwa kutilia maanani kuwa kumekuwepo na ushindani mkali kati ya nchi mbalimbali hasa kati ya China na Japan kwa ajili ya kujizatiti kiuchumi barani Afrika.
Katika kipindi cha mkutano wa TICAD, maafisa wakuu wa nchi za Afrika na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na maafisa wa Japan walizingatia mihimili mitatu mikuu ya jinsi ya kuimarisha amani na utulivu, kutatua masuala ya kiuchumi na matatizo na kujaribu kutafuta masuluhisho ya kijamii barani Afrika.
Ripoti zilizochapishwa zinaonyesha kuwa nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na ukosefu wa usalama, umaskini, masuala yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, migogoro ya afya, hali ya kisiasa isiyo imara, kasi ya ukuaji wa ukosefu wa ajira na mfumuko wa bei, matatizo ambayo yameathiri mchakato mzima wa maendeleo ya bara hili.
Matatizo ya nchi za Kiafrika yanaongezeka katika hali ambayo nchi hizi zina uwezo mkubwa kama vile rasilimali na utajiri mkubwa, idadi ya vijana na nafasi maalum za kijiografia. Kwa hiyo, nchi mbalimbali za bara hili, hasa katika miaka ya hivi karibuni, zimekuwa uwanja wa ushindani wa nchi nyingine za dunia kwa ajili ya kunufaika na uwezo huo. Kwa hakika, bara la Afrika ambalo huko nyuma lilidhurika kutokana na ukoloni wa Magharibi, sasa limekuwa uwanja wa makabiliano na maonyesho ya uwezo wa kiuchumi kati ya China na Japan.
Kuhusu suala hili, na katika mkutano uliomalizika karibunbi, Japan na nchi za Afrika zimekubaliana juu ya kuimarisha ushirikiano ili kudhamini maendeleo endelevu na kustawisha migodi ya madini muhimu. Rasilimali hizi ni pamoja na cobalt, ambayo hutumika katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, na ambayo ina mchango muhimu katika kufikia malengo ya kuondoa hewa chafu ya kaboni duniani.
Vile vile, nchi za Afrika na jamii ya kimataifa zimeahidi kushirikiana kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za maendeleo ya bara hili, ambapo moja ya ushirikiano huu, ni kustawisha rasilimali watu na mafunzo ya wafanyakazi wenye ujuzi barani Afrika.
Wakati ushindani kati ya mataifa yenye nguvu duniani unaendelea kwa ajili ya kuwa na ushawishi wa kiuchumi na kisiasa barani Afrika, nchi nyingi za bara hili, zikiwa na mwamko wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, hazivumilii tena siasa za ukoloni na mitazamo ya uonevu, ambapo sasa zinataka ushirikishwaji uliosimama kwenye misingi ya kuheshimiana na haki sawa. Kuhusu suala hili, inaonekana kwamba nchi za Kiafrika karibuni sio tu zitaibuka zaidi na zaidi kama wadau muhimu wa kiuchumi katika ngazi ya kimataifa, bali pia ushawishi na nguvu yao ya kisiasa itakuwa na taathira kubwa katika maamuzi ya kimataifa. Sisitizo la Japan la kuendeleza ushirikiano wake na nchi za Afrika linapaswa pia kutathminiwa katika mtazamo huo.