Oct 15, 2021 04:22 UTC
  • Leo Ijumaa, ni siku ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Askari AS

Ijumaa ya leo inayosadifiana na mwezi 8 Mfunguo Sita 1443 Hijria ni siku ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hasan al Askari, Imam wa 11 wa Waislamu wa Kishia duniani.

Siku kama ya leo mwaka 260 Hijria, Imam Hasan al Askari, mmoja wa wajukuu watoharifu wa Bwana Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi huko Samarra, kaskazini mwa Iraq.

Baba wa Imam huyo wa 11 kati ya Maimamu 12 wa kizazi kitoharifu cha Mtume Muhammad SAW alikuwa ni Imam Hadi AS na mama yake alikuwa ni bibi mwema, mwenye elimu nyingi na aliyejaa sifa za uungwana.

Baada ya kuuliwa shahidi baba yake, Imam Hasan al Askari alichukuwa jukumu zito la kuongoza Waislamu na kulinda dini tukufu ya Mwenyezi Mungu.

Mamia ya maelfu ya wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume hujitokeza katika kumbukumbu kama hizo

 

Katika umri wake mfupi lakini uliojaa baraka, mtukufu huyo alilea wanafunzi wengi wasomi na waliojaa fadhila za kimaadili na kidini na kila mmoja wao alikuwa bahari ya elimu na alitoa mchango mkubwa katika kuiendeleza na kuidumisha dini tukufu ya Kiislamu.

Umri wa miaka 29 wa Imam Hasan al Askari AS uligawika kwenye awamu tatu. Awamu ya miaka 13 ya kwanza ya umri wake ambao aliupitishia mjini Madina, awamu ya miaka 10 aliyoipitishia Samarra kaskazini mwa Iraq na awamu ya tatu ya takriban miaka 6 ya kuwa kwake Imam wa Waislamu.

Imam Hasan al Askari ndiye baba wa Imam wa Zama, Imam Mahdi AS. Tunatoa mkono wa pole kwa wapenzi wote wa Ahlul Bayt wa Mtume na kila mpenda haki duniani kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyouawa shahidi Imam Hasan al Askari AS.

Tags