May 22, 2016 16:20 UTC
  • Waziri Mkuu mpya Uturuki aahidi kuongezewa mamlaka rais

Binali Yildirim, Waziri wa Uchukuzi wa Uturuki ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa chama tawala AKP sambamba na kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo kuchukua nafasi ya Ahmet Davutoğlu.

Yildirim ameahidi kuwa atashinikiza kufanyiwa marekebisho katiba ya nchi ili kubadili mfumo wa uongozi kutoka ule wa bunge na kuwa na mfumo wa rais, ambao unampa mamlaka zaidi rais wa nchi.

Akiwahutubia wafuasi wa chama tawala mjini Ankara baada ya kuchaguliwa, Waziri Mkuu mpya wa Uturuki amesema: "Suluhu ya mkanganyiko wa kisiasa unaoshuhudiwa hivi sasa nchini ni kupatikana katiba mpya na kuwa na mfumo wa rais, mambo hayatakua namna yalivyo iwapo rais atachaguliwa na wananchi moja kwa moja."

Binali Yildirim ambaye ni mpambe wa karibu wa Rais Recep Tayyip Erdogan na mmoja wa waasisi wa chama cha AKP, amechaguliwa kwa kura zote 1,405 za wajumbe wa chama hicho tawala, katika kongamano la dharura la chama hicho cha Uadilifu na Ustawi.

Haya yanajiri siku chache baada ya Ahmet Davutoğlu, kutangaza rasmi kujiengua katika uongozi wa chama tawala cha Uadilifu na Ustawi (AKP) na hivyo kulazimika pia kuachia madaraka ya Uwaziri Mkuu. Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, Davutoğlu alilazimika kuchukua uamuzi huo ikiwa ni kusalimu amri mbele ya takwa la Rais Recep Tayyip Erdoğan la kutaka kuongezwa mamlaka ya rais.

Tags