WHO: Idadi halisi ya waliofariki kwa Covid-19 ni mara mbili au tatu zaidi ya takwimu rasmi
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, kwa kuzingatia vifo vinavyosababishwa moja kwa moja na virusi vya corona na vile vinavyotokana na virusi hivyo kwa njia isiyo ya moja kwa moja, idadi halisi ya vifo hivyo inaweza kuwa kubwa mara mbili au tatu zaidi ya takwimu rasmi.
Wakati takwimu rasmi za vifo vinavyosababishwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Covid-19 imepindukia milioni tano duniani kote, WHO imetangaza kuwa, idadi halisi ya vifo hivyo inaweza ikawa kubwa mara mbili au tatu zaidi ya takwimu rasmi.
Kwa mujibu wa gazeti la kila wiki la Economist, virusi vya corona vimesababisha vifo vya watu wapatao milioni 17 duniani, lakini pamoja na hayo, idadi kamili ya watu waliofariki kutokana na virusi hivyo na ndogo mno ikilinganishwa na ya baadhi ya majanga mengine makubwa ya mripuko yaliyowahi kutokea duniani, ikiwemo kwa mfano homa ya mafua ya Uhispania iliyotokea katika miaka ya 1918 hadi 1919 na kusababisha vifo vya watu milioni 50 hadi 100 duniani.

Kituo cha utafiti cha Pasteur nchini Ufaransa nacho pia kimelizungumzia suala hilo na kueleza kwamba, katika kipindi kifupi, corona imesababisha vifo vya watu wengi, lakini kama Shirika la Afya Duniani lisingechukua hatua na tahadhari za kiafya ikiwemo kuweka kafyu, kusimamisha shughuli mbalimbali na kutoa chanjo, hali ya mafaa ingekuwa mbaya zaidi.../