Vikwazo vya Upande mmoja, kizuizi cha malengo ya ustawi endelevu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i76808-vikwazo_vya_upande_mmoja_kizuizi_cha_malengo_ya_ustawi_endelevu
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani vinazizuia nchi mbalimbali kupata vyanzo vya fedha na ustawi unaohitajika kwa ajili ya kutimiza malengo ya ustawi endelevu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 12, 2021 00:10 UTC
  • Vikwazo vya Upande mmoja, kizuizi cha malengo ya ustawi endelevu

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani vinazizuia nchi mbalimbali kupata vyanzo vya fedha na ustawi unaohitajika kwa ajili ya kutimiza malengo ya ustawi endelevu.

Majid Takht-Ravanchi ambaye amehutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokutana kujadili suala la kulinda amani na usalama wa kimataifa, aliashiria uraibu wa Marekani wa kuziwekea vikwazo nchi mbalimbali na kusema kuwa, masuala kama umaskini, ukosefu wa usawa na uadilifu vinaweza kuwa chachu ya kushadidi migogoro na machafuko na kudhoofisha jitihada za kuimarisha amani endelevu katika nchi zinazosumbuliwa na mizozo.

Katika miongo ya karibuni vikwazo vimekuwa vikitumiwa na madola yenye nguvu kama fimbo na wenzo wa kuzishinikiza nchi nyingine katika uwanja wa kimataifa. Tangu mwanzoni mwa muongo wa 1990 Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zilizoendelea kiviwanda zimetekeleza mamia ya vikwazo dhidi ya nchi mbalimbali. Vikwazo hivyo vimekuwa vikiwekwa kwa kutumia visingizio mbalimbali kama kuzuia kuenea silaha za nyuklia, haki za binadamu na kadhalika. Hata hivyo ukweli ni kwamba, vikwazo vya nchi hizo za Magharibi huwekwa kwa malengo ya kisiasa, kupenda kujitanua na sera za mabavu na ujuba. Raisi wa zamani wa Marekani, Woodrow Wilson aliwahi kusema kuwa: "Taifa linalowekewa vikwazo litasalimu amri au kuzingirwa; Tumieni wenzo huu wa kiuchumi wa amani, wa kimya na angamizi, na hakuna haja kutumia nguvu za jeshi."  

Woodrow Wilson

Hata hivyo dunia nzima inajua jinsi vikwazo hivyo vinavyokanyaga haki za binadamu, vinavyowaathiri wananchi wa kawaida na wasio na hatia yoyote. Utafiti wa wachumi Matthias Novinkirsch na Florian Neumeier kuhusu athari za vikwazo kwa nchi tofauti unaonesha kuwa, vikwazo vinasababisha ukosefu wa usawa na uadilifu katika mapato, umaskini na kupunguza uzalishaji ghafi wa ndani ya nchi zinazolengwa. Kwa mfano tu vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi mbalimbali baina ya miaka 1991 na 2018 vimezidisha umaskini katika nchi zilizolengwa kwa karibu asilimia 3.5. Vilevile ulisababisha kushuka chini uzalishaji wa nchi hizo kwa zaidi ya asilimia 2.

Vilevile vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyotekelezwa mwaka 1976 hadi 2012 vimepelekea kupungua uzalishaji ghafi wa ndani ya nchi zilizolengwa kwa asilimia 25.5.

Nchi ya Iran ambayo imekuwa ikilengwa kwa vikwazo vya miaka mingi vya nchi za Magharibu hususan Marekani imeathiriwa na vikwazo hivyo, na sehemu ya vyanzo vya fedha vya serikali ama imefutwa au kuzuiwa; suala ambalo limezidisha mashinikizo ya kiuchumi kwa wananchi. Hivyo haiwezekani kabisa kukubali madai ya nchi hizo zinazotumia wenzo wa vikwazo kwamba, havina taathira yoyote kwa raia na wananchi wa kawaida. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, moja kati ya sababu za vikwao vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran ni kutaka kuwashinikiza viongozi kwa kuzidisha mbinyo na matatizo ya wananchi.

Jawad Salehi Isfahani ambaye ni mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Virginia Tech huko Marekani anasema kuhusu taathira mbaya za vikwazo vya kuanzia mwaka 2010 hadi 2029 dhidi ya Iran kwamba: Familia za maeneo ya vijijini zimeathiriwa zaidi na vikwazo hivyo. Mwaka 2010 kiwango cha umaskini katika maeneo ya vijijini kiliongezeka maradufu na katika maeneo ya mijini kimeongezeka kwa asilimia 60. Rekodi nzuri ya Jamhuri ya Kiislamu ya kupunguza umaskini hadi hadi nusu iliathiriwa sana na vikwazo hivyo kutokana na na kupungua kwa pato la taifa, vilevile kutokana na vikwazo vya serikali ya Donald Trump dhidi ya Iran vilivyoandamana na kipindi cha maambukizi makali ya virusi vya corona."

Nukta muhimu ya kizingatiwa ni kuwa vikwazo katika upande mmoja, hupelekea kupungua sana mahitaji ya awali ya wananchi na kuzuia nchi upata vyanzo vya fedha zinazohitajika kwa ajili ya ustawi, na katika upande mwingine ni miongoni mwa sababu kuu za kuendelea na kushadidi mizozo katika maeneo mbalimbali ya dunia. Kwa sababu hiyo kuna udharura wa kuwepo ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja.

Kwa sababu hiyo, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, kuna udharura wa kukabiliana na hatua za kujichukua maamuuzi ya upande mmoja ikiwa ni pamoja vikwazo na uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya nchi nyingi ili kuweza kuzuia ipasavyo mizozo inayojitokeza baina ya nchi na katika maneo mbalimbali.