May 24, 2016 16:21 UTC
  • Chama chenye misimamo mikali Ujerumani chavunja mazungumzo na Waislamu

Chama cha mrengo wa kulia nchini Ujerumani cha AfD kimevunja mazungumzo yaliyotazamia kuupatia ufumbuzi mkwaruzano kati yao na wanaharakati Waislamu nchini humo.

Frauke Petry, Mkuu wa chama hicho chenye misimamo ya kufurutu ada amesema wamelazimika kuondoka kwenye meza ya mazungumzo hayo baada ya msomi mashuhuri wa Kiislamu kukataa kufuta kauli yake ya awali, ya kukifananisha chama hicho na chama cha kinazi cha Adolf Hitler.

Mwezi uliopita, Aiman Mazyek, muasisi wa mazungumzo hayo aliifananisha misimamo ya chama cha AfD na ile ya kinazi ya Adolf Hitler; baada ya chama hicho cha mrengo wa kulia kutoa wito wa kupigwa marufuku minara ya Misikiti, vazi la stara la burqa sambamba na kuvitaka vyombo vya usalama kudhibiti Misikiti na taasisi za elimu za Kiislamu.

Aidha chama hicho kimekuwa kikiitaka serikali ya Ujerumani kutoruhusu wahamiaji na wakimbizi kuingia nchini mbali na kueneza propaganda za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Chama hicho kilimjia juu Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa 'kuwafungulia mlango' wakimbizi haswa wanaokimbia mapigano nchini Syria.

Hii ni katika hali ambayo, asilimia 5 ya Wajerumani ambao ni sawa na watu milioni 4 wa nchi hiyo ya Ulaya yenye jumla ya watu wapatao milioni 80 ni Waislamu.

Tags