Lavrov: Haiyumkiniki Russia kujiunga na shirika la kijeshi la NATO
https://parstoday.ir/sw/news/world-i78524-lavrov_haiyumkiniki_russia_kujiunga_na_shirika_la_kijeshi_la_nato
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema haiyumkiniki nchi hiyo kujiunga na shirika la kijeshi la NATO.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Dec 28, 2021 02:42 UTC
  • Lavrov: Haiyumkiniki Russia kujiunga na shirika la kijeshi la NATO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema haiyumkiniki nchi hiyo kujiunga na shirika la kijeshi la NATO.

Sergey Lavrov amesisitiza kuwa, haiwezekani Russia kuwa mwanachama wa NATO kwa sababu Wamagharibi hawataki wawe na mshindani yeyote duniani.

Lavrov ametoa matamshi hayo wakati mivutano kati ya Russia na NATO ikiwa inaendelea huku kukiwepo na ripoti kuhusu azma ya Finland, Sweden na hata Ukraine kutaka kujiunga na shirika hilo la kijeshi la Magharibi.

Siku ya Jumamosi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova alitoa onyo juu ya matokeo hasi ya kisiasa na kijeshi yatakayoshuhudiwa endapo Finland na Sweden zitakuwa wanachama wa NATO.

Sergey Lavrov

Tarehe 17 Desemba, wizara ya mambo ya nje ya Russia ilitoa rasimu ya mikataba iliyopendekezwa na nchi hiyo kwa Marekani na shirika la kijeshi la NATO kuhusu hakikisho la usalama kwa pande hizo tatu.

Kwa mujibu wa vifungu vya rasimu hiyo, Russia na NATO zitapaswa ziahidi kuwa hazitaweka makombora ya masafa ya kati na masafa mafupi katika maeneo yanayoweza kutumika kushambulia upande wa pili.

Pande hizo mbili pia zitapaswa kuhakikisha haziandai mazingira yanayoweza kutafsiriwa kuwa ni tishio kwa upande wa pili.

Kupitia rasimu hiyo, Russia imependekeza pia kwa NATO kwamba ziwe zikibadilishana taarifa kila mara kuhusiana na mazoezi na manuva ya kijeshi ambayo kila upande unakusudia kufanya.../