Poland yaonya: Ulaya ipo katika ncha ya kutumbukia vitani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland ametahadharisha kuwa, bara Ulaya lipo katika hatari kubwa ya kutumbukia kwenye vita wakati huu, kuliko ilivyokuwa miongo mitatu iliyopita.
Zbigniew Rau alitoa indhari hiyo jana Alkhamisi akiwahutubia wajumbe wa Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano ya Ulaya (OSCE) na kuongeza kuwa, "Kwa wiki kadhaa sasa, tunakabiliwa na hatari ya kutokea makabiliano ya kijeshi Mashariki mwa Ulaya."
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Poland amebainisha kuwa, "Inaelekea kuwa, hatari ya (kuibuka) vita katika eneo la Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano ya Ulaya (OSCE) ni kubwa mno, zaidi ya ilivyokuwa miaka 30 iliyopita."
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) ameonya pia kuhusu uwezekano mkubwa wa kuibuka vita barani Ulaya.

Jens Stoltenberg alisema hayo baada ya kutofikiwa tija ya maana kwenye mkutano ulojiri kwa muda wa saa nne wa Baraza la NATO-Russia (NRC) kuhusu mzozo wa Ukraine.
Amesema utesi mkubwa ungalipo katika suala tata la kuruhusiwa au kutoruhusiwa Ukraine kujiunga na muungano wa kijeshi wa NATO, unaoongozwa na Marekani.