"CIA ilifahamu kuhusu njama za kumpindua Rais wa Venezuela"
(last modified Sun, 30 Jan 2022 07:52:37 GMT )
Jan 30, 2022 07:52 UTC

Imebainika kuwa, maafisa wa ngazi za juu wa utawala wa Marekani wakiwemo maafisa waandamizi wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA, walifahamu kuhusu kuwepo kwa njama za kumpindua madarakani Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.

Hayo yamefichuliwa na jenerali mstaafu wa jeshi la Venezuela, Cliver Alcala ambaye aliongoza katika upangaji wa njama hizo zilizogonga mwamba.

Alcala amefichua hayo kupitia mawakili wake wanaotaka kufutwa mashitaka dhidi ya jenerali huyo mstaafu, yaliyofunguliwa karibu miaka miwili iliyopita na waendesha mashitaka wa US mjini New York, wakimtuhumu kwa ugaidi wa magendo ya mihadarati.

Mawakili wa afisa huyo wa zamani wa kijeshi wa Venezuela wamesema, jitihada za kuupindua utawala wa Maduro unajulikana vizuri na serikali ya Marekani, na kwamba "upinzani wake kwa utawala wa (Maduro) na juhudi za kuupindua uliripotiwa kwa afisi za juu za Marekani, ikiwemo CIA, Baraza la Usalama wa Taifa, na Wizara ya Fedha."

Rais Maduro (kulia) na Juan Guaido

Nyaraka hizo za mahakama zimeibua masuali mengi kuhusu nafasi ya utawala uliopita wa Donald Trump katika njama hizo zilizofeli za kutaka kumpindua Rais Maduro mnamo Mei mwaka 2020.

Ikumbukwe kuwa, Juan Guaido kiongozi wa upinzani wa Venezuela Januari 23 mwaka 2019 alijitangaza kuwa Rais wa Venezuela na Marekani ikamtambua rasmi mara moja baada ya tangazo hilo, kitendo ambacho Washington ilidhani kingeandaa mazingira ya kupinduliwa Maduro.

 

Tags