Trump: Nitawasamehe waliovamia Kongresi ya Marekani nikishinda urais
Aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump amesema iwapo atagombea na kushinda urais katika uchaguzi wa mwaka 2024, atawasamehe na kuagiza kuachiwa huru watenda jinai waliohusika na shambulizi dhidi ya jengo la Kongresi mnamo tarehe 6 Januari mwaka jana, lililofanywa na wafuasi wake.
Trump amesema hayo katika mkutano wa kisiasa huko Conroe, Texas, ingawaje hajaweka wazi iwapo atagombea urais au la katika uchaguzi ujao, baada ya kubwagwa na Joe Biden katika uchaguzi uliopita wa 2020.
Amesema wafuasi hao ambao wameshahukumiwa na wanatumikia kifungo jela kwa uhalifu waliofanya, hawatendewi uadilifu na utawala wa Biden, na kwamba atawapa msahama akishinda uchaguzi ujao wa rais.
Ikumbukwe kuwa, kikao cha Kongresi ya Marekani ambacho kilifanyika kwa lengo la kupasisha ushindi wa uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020 huko Marekani kilikabiliwa na shambulio la wafuasi wa Trump na kusimama kwa masaa kadhaa.
Watu wasiopungua watano wakiwemo maafisa usalama wa nchi hiyo waliuawa katika shambulio hilo la kutisha, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.
Weledi wa mambo wanasema shambulizi hilo dhidi ya jengo la Kongresi tarehe 6 Januari 2020 ulikuwa uasi uliochochewa na Donald Trump, na ilikuwa hujuma dhidi ya Kongresi, Katiba na demokrasia.