Erdogan: Rais wa Israel ataitembelea Uturuki mwezi ujao
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema rais wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Isaac Herzog ataitembelea nchi hiyo mwezi ujao wa Machi.
Erdogan amesema hayo leo Alkhamisi katika kikao na waandishi wa habari, kabla ya safari yake ya kwenda Ukraine na kueleza kuwa, Herzog atafanya ziara rasmi ya kuitembelea Uturuki katikati ya mwezi ujao wa Machi.
Kauli ya Erdogan imekuja siku chache baada ya wananchi wa Uturuki kufanya maandamano makubwa nje ya ubalozi mdogo wa Israel mjini Istanbul, kupinga na kulaani safari hiyo tarajiwa ya rais wa utawala haramu unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mambo yenye jumbe zisemazo “Wauaji wa watoto Wapalestina ondokeni Palestina” na “Hatumtaki Rais wa Israel nchini kwetu.”
Wananchi wa Uturuki wamesema safari ya Rais wa Israel nchini humo ni pigo kwa umma wote wa Kiislamu na hususan wananchi madhulumu wa Palestina wanaopigania uhuru wao.
Wadadisi wa mambo wanasema, hivi sasa kutokana na mgogoro wa kiuchumi, serikali ya Rais Erdogan wa Uturuki imeamua kupuuza kadhia ya Palestina na kujikurubisha kwa utawala haramu wa Israel kwa ajili ya maslahi yake ya kitaifa.