Guterres apuuza mashinikizo ya US ya kutaka asusie Olimpiki China
(last modified Thu, 03 Feb 2022 12:42:14 GMT )
Feb 03, 2022 12:42 UTC
  • Guterres apuuza mashinikizo ya US ya kutaka asusie Olimpiki China

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepuuzilia mbali mwito wa Balozi wa Marekani katika umoja huo wa kumtaka asusie hafla ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi kali nchini China.

Licha ya mashinikizo hayo ya Marekani na nchi nyingine za Magharibi, lakini Guterres anatazamiwa kushiriki ufunguzi wa Michezo hiyo ya kimataifa ya Olimpiki ya Beijing kesho Ijumaa.

Katibu Mkuu wa UN amekuwa akisisitiza kuwa, matukio ya aina hii ya michezo yana umuhimu mkubwa katika kuwakurubisha pamoja watu wa jamii mbalimbali duniani.

Guterres ametupilia mbali wito huo wa Linda Thomas-Greenfield, Balozi na Mwakilishi wa Marekani UN na kueleza kuwa, "Michezo ya Olimpiki inapaswa kuwa nembo ya amani duniani."

Serikali ya Joe Biden imesema haitatuma mwakilishi rasmi au wa kidiplomasia katika Michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi nchini China, eti kutokana na mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya binadamu katika mkoa wa Xinjiang na vitendo vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu China.

Hii ni katika hali ambayo, nchini Marekani kwenyewe wananchi hususan Wamarekani wenye asili ya Afrika wanakumbwa na hali mbaya sana ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Wanamichezo karibu elfu tatu wa nchi mbalimbali duniani wanatazamiwa kushiriki kwenye mashindano hayo ya kimataifa mjini Beijing, nchini China kuanzia kesho Ijumaa na Februari 20.