Rais wa Ukraine: Wako wapi waliotuhakikishia kuwa watatudhaminia usalama wetu?
(last modified Fri, 25 Feb 2022 12:55:27 GMT )
Feb 25, 2022 12:55 UTC
  • Rais wa Ukraine: Wako wapi waliotuhakikishia kuwa watatudhaminia usalama wetu?

Rais wa Ukraine mwenye mielekeo ya Magharibi ameikiri kuwa amebaki peke yake kwa ajili ya kukabiliana na Russia, kufuatia msambaratiko wa uungaji mkono dhaifu wa Magharibi na kuingia vikosi vya jeshi la Russia katika mji mkuu wa nchi hiyo.

Baada ya kuanza vita na mapigano baina ya vikosi vya jeshi la Russia na Ukraine, na huku zikitangazwa habari za kutatanisha kuhusu kutekwa mji mkuu wa Ukraine Kiev, waungaji wa Kimagharibi wa Ukraine wametosheka na utoaji kauli za vitisho tu vya kuiwekea Moscow vikwazo zaidi vya kiuchumi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amehutubia kupitia televisheni akisema: "Sisi hatuiogopi Russia, lakini kitu gani kinaidhaminia usalama nchi yetu? Ziko wapo zile pande na nchi zinazotupa hakikisho hilo?"

Katiba hotuba yake hiyo aliyotoa alfajiri ya kuamkia leo Zelensky amezikosoa kwa njia isiyo ya moja kwa moja nchi za Magharibi akisema: "wametuacha peke yetu katika vita na Russia."

Wakati huohuo wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon imetangaza kuwa, kutokana na kushtadi vita na mapigano nchini Ukraine, nchi hiyo inatuma askari wake wengine elfu saba barani Ulaya.

Askari wa Ukraine

Askari hao, ambao wanajumuisha wapiganaji na wa vikosi vya utoaji huduma na msukumo watawekwa nchini Ujerumani kutumika kama kikosi cha ngao ya kuwalinda na hujuma za Russia waitifaki wa Washington katika shirika la kijeshi la NATO na kujiweka tayari pia kwa ajili ya kutoa msaada wa aina yoyote utakaohitajika katika eneo hilo.

Kabla ya uamuzi huo wa sasa, Marekani ilikuwa tayari imeshatuma askari wengi katika nchi jirani na Ukraine za Romania na Poland huku ikiituhumu Russia kuwa imekusanya zaidi ya askari laki moja na elfu arubaini katika mpaka wake wa pamoja na Ukraine na kuanzisha chokochoko katika eneo la mashariki la Donbas ili kupata kisingizio cha kuivamia na kuishambulia kijeshi nchi hiyo.../