WHO yatahadharisha kuhusu uhaba wa oksijeni katika hospitali za Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i80854-who_yatahadharisha_kuhusu_uhaba_wa_oksijeni_katika_hospitali_za_ukraine
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha juu uhaba wa mitungi ya oksijeni katika hospitali za Ukraine katika kipindi cha masaa 24 yajayo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Feb 28, 2022 04:19 UTC
  • WHO yatahadharisha kuhusu uhaba wa oksijeni katika hospitali za Ukraine

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha juu uhaba wa mitungi ya oksijeni katika hospitali za Ukraine katika kipindi cha masaa 24 yajayo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa hospitali nchini Ukraine huenda zikakosa huduma ya oksijeni katika masaa 24 yajayo kufuatia mashambulizi ya Russia kuvuruga huduma za usafiri kote nchini humo; na hivyo kuyaweka hatarini maisha ya maelfu ya watu. 

Katika taarifa yake ya jana, WHO imesema kuwa malori yameshindwa kusafirisha oksijeni kutoka viwandani hadi mahospitalini huko Ukraine ikiwemo katika mji mkuu Kiev ambao unakabiliwa na wimbi la mashambulizi ya makombora ya Russia. 

Dakta Tedros Adhanom Gebreyesus Mkurugenzi Mkuu wa WHO na Hans Kluge Mkurugenzi wa shirika hilo barani Ulaya wamesema katika taarifa yao ya pamoja kwamba, "aghalabu ya hospitali zinaweza kumaliza akiba yao ya oksijeni ndani ya saa 24 zijazo. Baadhi ya hospitali zimeishiwa na huduma ya oksijeni; hali inayoyaweka hatarini maisha ya maelfu ya raia wa Ukraine. " 

Shirika la Afya Duniani limesema kuwa sasa Ukraine inahitaji ongezeko la asilimia 25 ya huduma ya oksijeni ikilinganishwa na mahitaji ya nchi hiyo kabla ya kushambuliwa na Russia wiki iliyopita. Tedros na Kluge wamesema, "ni muhimu kuhakikisha kwamba vifaa vya matibabu vya kuukoa maisha ikiwa ni pamoja na hewa ya oksijeni vinawafikia wahitaji."

Uhaba wa oksijeni Ukraine