Russia: Lazima Ukraine ipokonywe silaha na isiwe na nguvu za kijeshi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema, nchi yake inataka iwepo orodha ya silaha ambazo Ukraine haitaweza katu kuwa na nazo na wala hazitatengenezwa nchini humo.
Sergey Lavrov amesisitiza kwa mara nyingine tena kuhusu ulazima wa Ukraine kupokonywa silaha na akasema, inapasa wananchi wa Ukraine waamue kuhusu mustakabali wao.
Halikadhalika, Lavrov amekanusha kama Russia ina nia ya kuihodhi Ukraine na akasisitiza kwamba, nchi yake iko tayari kwa mapatano ya kufikia njia ya ufumbuzi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameeleza kuwa, kuna uhakika mwingi wa mambo unaothibitisha kuwa Ukraine ni sehemu ya mpango wa Magharibi wa kuanzisha "ukanda wa kiuadui" wa kuizunguka Russia na kwamba, kwa muda wa miaka miwili sasa, nchi hiyo imekuwa ikisheheneshwa silaha, ambapo katika miezi ya karibuni shehena za zana za kijeshi zimeongezeka nchini humo kwa kiwango kikubwa.
Lavrov amevilaumu pia vyombo vya habari na wanasiasa wa nchi za Magharibi kwa kufumbia macho matatizo na mateso ya watu wa eneo la Donbas, ambao amesema "wameshambuliwa na kuuawa kwa makombora kwa muda wa miaka minane" na akaongeza kuwa, lengo jengine kuu inalofuatilia Russia huko Ukraine ni "kuondoa uajinabia".
Baada ya viongozi wa maeneo yaliyojitangazia uhuru ya Donetsk na Luhansk mashariki ya Ukraine kuiomba Russia iwatumie misaada ya kijeshi kulingana na mikataba ya ushirikiano iliyoko baina yao, siku ya Alkhamisi ya tarehe 24 Februari, Rais Vladimir Putin wa Russia alitangaza kuanza operesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbas ziliko jamhuri hizo mbili zilizojitenga na Ukraine.../