Ripoti: Yamkini mgogoro wa Ukraine ukaiingiza Marekani na Russia vitani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i81070-ripoti_yamkini_mgogoro_wa_ukraine_ukaiingiza_marekani_na_russia_vitani
Huku Marekani na waitifaki wake wakiendelea kuichochea Ukraine ili ikabiliane na oparesheni za kijeshi za Russia ndani ya nchi hiyo, maafisa wa Marekani wameingiwa na wasiwasi mkubwa kuwa kuna uwezekano wa makabiliano baina ya wanajeshi wa Russia na Marekani na hilo linaweza likapelekea kuibuka vita vikubwa baina ya pande hizo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Mar 06, 2022 04:28 UTC
  • Ripoti: Yamkini mgogoro wa Ukraine ukaiingiza Marekani na Russia vitani

Huku Marekani na waitifaki wake wakiendelea kuichochea Ukraine ili ikabiliane na oparesheni za kijeshi za Russia ndani ya nchi hiyo, maafisa wa Marekani wameingiwa na wasiwasi mkubwa kuwa kuna uwezekano wa makabiliano baina ya wanajeshi wa Russia na Marekani na hilo linaweza likapelekea kuibuka vita vikubwa baina ya pande hizo.

Gazeti la Business Insider limeandika kuwa, hatua ya Marekani  na waitifaki wake kuunga mkono Ukraine kijeshi katika makabiliano na Russia inamaanisha kuwa, ndege zao za kivita zinatekeleza oparesheni karibu na Ukraine eneo ambalo pia kuna ndege za kivita za Russia na kuna uwezekano mkubwa wa kufanyika kosa ambalo litawasha moto wa vita.  

Afisa mmoja wa kijeshi wa Marekani amenukuliwa na gazeti hilo akisema Marekani ina njia kadhaa za kuwasiliana na Russia kuhusu masuala hatari iwapo hali ya dharura itajitokeza. Amesema kuanzia Machi 1, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilianzisha laini maalumu ya siri ya kuwasiliana na Wizara ya Ulinzi ya Russia kwa lengo la kuzuia ajali za kijeshi na hali ya taharuki kuenea.

Ripoti hiyo imesema tayari NATO imeimarisha vikosi vyake Ulaya Mashariki hasa katika Bahari Nyeusi na Poland.

Marekani na nchi zingine za NATO zimekuwa zikituma misaada ya kijeshi Ukraine lakini zimejizuia kuingia vitani moja kwa moja kwa kuhofia kuwa hatua kama hiyo itaibua magogoro na Russia utakaowasha moto wa vita kote Ulaya na Marekani.

Hayo yanaripotiwa wakati ambao Idara ya Usalama wa Nje ya Russia- SVR RF- imefichua kuwa, Marekani inawasafirisha magaidi wa ISIS au Daesh kutoka Syria na kuwaingiza Ukraine.

Rais wa Russia, Vladimir Putin Alhamisi tarehe 24 Februari aliamuru operesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbass kujibu ombi la msaada wa kijeshi kutoka kwa viongozi wa Jamhuri za Donetsk na Luhansk huko Mashariki mwa Ukraine. Russia imekuwa ikilalamika kwa muda mrefu kuwa, serikali yenye misimamo ya Kimagharibi ya Ukraine inalenga kujiunga na muungano wa kijeshi wa NATO unaoongozwa na Marekani na hilo ni tishio kubwa kwake.