UN: Hatuna taarifa za kuwepo silaha za biolojia nchini Ukraine
Naibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na udhibiti wa kuenea kwa silaha duniani amesema, umoja huo hauna taarifa zozote kuhusu mipango ya uzalishaji silaha za vijidudu za kibiolojia nchini Ukraine.
Izumi Nakamitsu ameyasema hayo alipohutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kufuatia ombi lililowasilishwa na Russia la kuchunguza madai kwamba Marekani na Ukraine zina mpango wa kuzalisha silaha za bilolojia ambazo ni "tishio dhidi ya amani na usalama wa kimataifa".
Bi. Nakamitsu amesema “tunatambua ripoti kutoka vyombo vya habari kuhusu madai ya uwepo wa mipango hiyo lakini Umoja wa Mataifa hauna taarifa.”
Amesema kutokuwepo kwa mipango hiyo kunatokana na uwepo wa Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 1972 kuhusu silaha za kibiolojia BWC, ambao unakataza kuendeleza, kuzalisha, kununua, kusafirisha, kuhifadhi na kutumia silaha za kibiolojia au za sumu.
Naibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na udhibiti wa kuenea kwa silaha duniani amesema, Russia na Ukraine zote ni wanachama wa mkataba huo na kwamba silaha za kibiolojia zimepigwa marufuku tangu mwaka 1975 mkataba huo ulipoanza kufanya kazi.
Hata hivyo amesema mkataba huo una kasoro ambazo zinapaswa kushughulikiwa ili uweze kuwa thabiti zaidi.
Bi. Nakamitsu amebainisha kuwa, ni kwa hali hiyo anazisihi nchi wanachama wa BWC kushiriki mkutano wa 9 wa tathmini ya mkataba huo uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu huko Geneva, Uswisi ili kuangalia upya mkataba ili uweze kukabili changamoto za sasa na zijazo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, wakati wa kikao hicho cha Baraza la Usalama, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa Nebenzia Vassily Alekseevich alieleza kuwa Marekani inasaidia mipango ya silaha za kibiolojia nchini Ukraine sambamba na mipango ya kutumia ndege wanaohamahama kusambaza virusi na vimelea vya magonjwa kama vile homa ya mafua ya ndege.
Amesema Russia imegundua kuna maabara za kibiolojia nchini Ukraine zenye vijidudu ambapo hatua zinafanyika kuviimarisha vijidudu hivyo vitumike kama silaha.
Hata hivyo Marekani na Ukraine zimekanusha madai hayo na kusisitiza kuwa ushirikiano wa kimaabara uliopo baina ya pande hizo mbili nchini Ukraine unahusu utafiti wa magonjwa kama vile COVID-19, tafiti ambazo zimedai zinasaidia kila mtu.../