Shutuma za Russia kwa Marekani inayokwamisha mazungumzo ya Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergeĭ Viktorovich Lavrov ameishutumu vikali Marekani kwa siasa zake kuhusu vita vya Ukraine na kusema kuwa, Washington ndiyo inayokwamisha kufikiwa makubaliano baina ya Moscow na Kyiv hata katika masuala madogo kabisa. Amesema, hivi sasa Marekani inawatwisha viongozi wa Ukraine misimamo yake na ndio maana Kyiv inakwamisha kila kitu katika mazungumzo yake na Russia.
Shutuma hizo za Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia dhidi ya Washington zimetolewa katika hali ambayo Marekani inajionesha kidhahiri kuwa ina hamu ya kufikiwa makubaliano ya kukomeshwa vita huko Ukraine.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hivi sasa Marekani inataka vita vya Ukraine viendelee ili nchi zote mbili za Russia na Ukraine zizidi kupata hasara. Wachambuzi hao wanasema kuwa, ni Marekani ndiyo iliyoichochea Ukraine iingie vitani na Russia na kuiahidi kuisaidia kwa kila kitu lakini imeitelekeza. Aidha ni Washington ndiyo ambayo hadi hivi sasa inaitwisha misimamo yake serikali inayopenda Umagharibi ya Kyiv, ili isilegeze kabisa misimamo yake katika mazungumzo na Russia.
Wachambuzi hao wanasema, lengo hasa la Marekani ni kuvifanya vita vya Ukraine vichukue muda mrefu na haishughulishwi na roho za watu zinazoendelea kutoka na hasara za kila upande zinazosababishwa na vita hivyo. Marekani imezidisha sana misaada ya kijeshi kwa Ukraine na imerundika silaha zake katika nchi zinazopakana na Russia na wakati huo huo imeiahidi Kyiv kuwa itaipa uanachama wa Jeshi la Nchi za Magharibi NATO, yote hayo yanazidi kuwakwamisha kwenye mtengo viongozi wapenda Umagharibi wa Ukraine na kuwafanya wazidi kung'ang'ania misimamo yao dhidi ya Russia.
Sasa hivi Marekani ndiye kiongozi wa kambi ya Magharibi na imechochea sana kuwekewa Russia vikwazo vikali na vikubwa mno ambavyo havijawahi kutokea katika historia yake. Ndoto ya muda mrefu ya Marekani ni kuidhoofisha na kuisambaratisha Russia. Inaonekana wazi kuwa Washington inahisi kwamba wakati wa kuidhoofisha Russia ndio huu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergeĭ Lavrov anasema kuhusu suala hilo kwamba, katika mazungumzo baina ya Moscow na Kyiv tunaona wazi kuwa viongozi wa Washington wanawatwisha viongozi wa Ukraine matakwa yao. Ni jambo lililo wazi kabisa kwamba Wamarekani hawataki vita vya Ukraine vimalizike.
Kwa kweli inaonekana wazi kwamba inachofanya Marekani ni kujaribu kurefusha vita vya Ukraine na kutoa pigo kwa watu na nguvu za kijeshi za Russia na wakati huo huo kutumia vikwazo vya kila namna dhidi ya Moscow ili kusambaratisha uchumi wa nchi hiyo na kupunguza umaarufu wa Rais Vladimir Putin nchini humo. Hata hivyo viongozi wa Russia inaonekana wana mtazamo tofauti na huo. Dmitry Medvedev, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia anasema: Uchumi wa Russia hauwezi kusambaratika kwa vikwazo vya nchi za Magharibi kwani Moscow inajua cha kufanya wakati wa vikwazo na mazingira magumu sana. Si hayo tu, lakini baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieni (Urusi ya zamani), Russia imepata marafiki wa kuaminika kama China, nchi za kusini mashariki mwa Asia na za bara la Afrika.
Amma jambo moja liko wazi kabisa nalo ni kwamba, kuendelea vita hivyo kuna madhara makubwa kwa uchumi wa Ukraine na miundombinu yake. Wimbi la wakimbizi wa Ukraine nalo ni kubwa huku taarifa zikisema kuwa wakimbizi hao wameshapindukia milioni 3 na laki tatu nje wa Ukraine na milioni 6.5 ndani ya nchi hiyo. Madhara ya vita hivyo ni makubwa sana kwa Ukraine kuliko kwa nchi nyingine yoyote. Ni jambo lililo wazi kuwa athari mbaya za vita hivyo zitaendelea kuonekana pia kwa nchi za Ulaya zinazopokea wakimbizi, mbali na matatizo mengi yanayozikabili nchi hizo za Ulaya kutokana na madhara ya kutofikiwa vizuri na nishati kama ya gesi na mafuta kutoka nchini Russia.
Kiujumla ni kwamba, vita vya Ukraine vina madhara ya kila upande, lakini inavyoonekana ni kuwa Marekani inapenda vita hivyo viendelee na haishughulishwi na madhara na hasara za pande zote za vita hivyo.