Biden: Tutamjibu Putin iwapo atatumia silaha za kemikali
(last modified Fri, 25 Mar 2022 08:05:23 GMT )
Mar 25, 2022 08:05 UTC
  • Joe Biden
    Joe Biden

Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza kuwa iwapo Rais Vladimir Putin wa Russia atatumia silaha za kemikali na kusababisha uharibifu mkubwa huko Ukraine Marekani itajibu hatua hiyo.

Biden ambaye alikuwa mjini Brussels, Ubelgji, Alhamisi usiku alizungumza na vyombo vya habari ambapo akijibu swali la mwandishi habari wa Associated Press kwamba je, Marekani ina ushahidi wa uhakika kuhusu uwezekeno wa Russia kutumia silaha za kemikali, alisema: "Siwezi kufichua taarifa za kiintelijinsia lakini iwapo Putin atatumia silaha hizo sisi tutamjibu; majibu haya yatategemea jinsi silaha hizo tajwa zitakavyotumiwa." 

Kuhusu uwezekano wa China kuisaidia Russia, Rais wa Marekani amesema: Beijing inajua vyema taathira mbaya za kiuchumi zitakazosababishwa na misaada yake kwa Russia katika vita dhidi ya Ukraine. Biden ameongeza  kuwa: Wiki iliyopita alifanya mazungumzo na Rais Xi Jinping wa China kuhusu suala hilo na walikuwa na mazungumzo ya wazi.   

Rais wa Marekani aidha amelitaka kundi la G-20 liifukuze Russia ndani ya kundi hilo. 

Jumanne wiki hii Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov alisema katika mahojiano na televisheni ya CNN kwamba, nchi hiyo haina azma ya kutumia silaha za nyuklia, lakini kanuni za nchi hiyo kuhusu matumizi ya silaha hizo zipo wazi. Ikulu ya Russia ya Kremlin ilisema nchi hiyo haitakuwa na chaguo jingine isipokuwa kutumia silaha za nyuklia iwapo uwepo wa taifa hilo utakabiliwa na vitisho.

Dmitry Peskov