China yaikosoa Magharibi kwa sera za kindumakuwili kuhusu haki za binadamu
China imezishutumu nchi za Magharibi kwa kutumia sera za kindumakuwili kwa kushughulikia kwa wakati haki za binadamu za watu wanaokimbia vita vya Russia na Ukraine na kupuuza haki za wakimbizi kutoka nchi za Mashariki ya Kati, Afrika na Amerika ya Kusini.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Wang Wenbin amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing kwamba, matukio ya hivi sasa barani Ulaya yanaonesha sera na mismamo ya kindumakuwili katika medani ya kimataifa kuhusu masuala kadhaa kama vile kadhia ya Palestina, licha ya jinai za uvamizi wa Israel ambazo ni sawa na mauaji ya kimbari, ubaguzi wa rangi, kushambuliwa kwa matukufu, na kukanyaga sheria za kimataifa.
Akiashiria matamshi ya Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, aliyempokea Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken siku ya Jumapili, Wang Wenbin amesisitiza kuwa kadhia ya Palestina haipaswi kutelekezwa au kusahaulika, na dhulma iliyoendelea kwa zaidi ya miaka 50 sasa dhidi ya taifa hilo inapaswa kukomeshwa.
Amesema China itaendelea kusimama kidete na watu wa Palestina.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China pia ametoa wito wa kuwepo umoja zaidi kati ya makundi ya Wapalestina, na kufanyika bidii kwa ajili ya maridhiano halisi ya ndani.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesisitiza kuwa, misimamo ya kindumakuwili ya kuwahurumia wakimbizi nchini Ukraine, huku ikiwapuuza wakimbizi kutoka nchi za Mashariki ya Kati, Afrika na Amerika ya Kusini, haikubaliki.

Akizungumzia operesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine, Wang Wenbin amesema haikubaliki kuwa na vigezo vya aina mbili tofauti kwa kutaja mashaka ya raia nchini Ukraine kuwa uhalifu wa kivita huku tukipuuza manyanyaso yaliyowapata raia nchini Afghanistan, Iraq na Syria.