Apr 01, 2022 03:25 UTC
  • IMF: Vikwazo dhidi ya Russia yumkini vitadhoofisha dola ya US

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeonya kuwa, vikwazo dhidi ya Russia huenda vikadhoofisha na kuipotezea umashuhuri sarafu ya dola ya Kimarekani.

Katika mahojiano na gazeti la Financial Times, Gita Gopinath, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IMF amesema vikwazo dhidi ya Russia huenda vikazilamisha baadhi ya nchi au mashirika kukhitari kufanya biashara kwa kutumia sarafu nyinginezo badala ya dola ya Marekani.

Amesema tayari baadhi ya nchi zimeanza kufanya mashauriano kuhusu njia za kutupilia mbali matumizi ya sarafu ya dola ya Kimarekani katika biashara, na badala yake zitumie sarafu nyinginezo au njia mbadala.

Russia na India kwa sasa zinaandaa mchakato wa kutumia sarafu za nchi hizo za Rupee na Rouble katika miamala yao ya kibiashara, huku kukiwa na ripoti kuwa, Moscow na Beijing zinajadili pia njia za kutupilia mbali matumizi ya sarafu ya dola ya Kimarekani.

Tarehe 24 Februari na kufuatia msimamo wa Magharibi wa kupuuza wasiwasi wa kiusalama wa Russia, nchi hiyo ilianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya Ukraine kwa lengo la kuipokonya silaha nchi hiyo.

Kufuatia operesheni hiyo, kambi ya Magharibi ikiongozwa na Marekani imeiwekea vikwazo vikali sana vya kiuchumi Moscow, ambavyo havijawahi kushuhudiwa katika historia ya Russia.  Hata hivyo vikwazo hivyo vimekuwa na taathira hasi pia kwa chumi za Wamagharibi wenyewe.

Tags