WHO: Karibu watu wote duniani wanavuta hewa chafu
(last modified Tue, 05 Apr 2022 07:23:27 GMT )
Apr 05, 2022 07:23 UTC
  • WHO: Karibu watu wote duniani wanavuta hewa chafu

Shirika la Afya Duniani limesema karibu watu wote duniani wanavuta hewa chafu ambayo haikidhi viwango vya shirika hilo na hivyo wanakodolewa macho na magonjwa na hatari ya kifo.

Maria Neira, Mkurugenzi wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira wa WHO amesema asilimia 99 ya watu duniani wanaishi kwenye maeneo yenye kiwango cha juu zaidi cha uchafuzi wa hewa kuliko kilichowekwa na shirika hilo, uchafuzi unaosababisha mamilioni ya vifo kila mwaka.

Amesema miji 6000 katika nchi 117 duniani inafuatilia ubora wa hali ya hewa, lakini watu wanaoishi katika miji hayo bado wanavuta hewa chafu yenye chembechembe za sumu kama nitrogen dioxide.

Kwa mujibu wa WHO, watu wapatao milioni saba hufariki dunia kila mwaka kutokana na janga la uchafuzi wa hewa. Takwimu zinaonesha kuwa, uchafuzi wa hewa husababisha vifo vya watu milioni 1.1 barani Afrika kila mwaka, na hivyo kuwa chanzo kikuu cha pili cha vifo barani humo.

Haya yanajiri wiki chache baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kusema kuwa, ulimwengu unajikongoja kuhusu janga la hali ya hewa huku nchi zilizostawi kiuchumi duniani zikiruhusu kuongezeka uchafuzi wa mazingira kupitia gesi ya carbon katika hali ambayo uchafuzi wa mazingira unapasa kupunguzwa kwa kiasi kikubwa.

Kuna matumaini kwamba kupunguzwa kwa kiwango kikubwa zaidi cha hewa chafu kunaweza kusaidia kuzuia ongezeko la viwango vya joto duniani, mbali na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu.