Apr 17, 2022 07:59 UTC
  • Waislamu 5 wajeruhiwa kwa kupigwa risasi msikitini nchini Canada

Watu watano wamejeruhiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi na wahalifu wasiojulikana nchini Canada, huku vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vikionekana kushtadi nchini humo.

David Rydzik, Msemaji wa Polisi katika eneo la Toronto amethibitisha kutokea shambulio hilo na kueleza kuwa, ufyatuaji risasi huo ulitokea jana usiku katika msikiti ulioko katika wilaya ya Scarborough.

Amesema milio sita ya risasi ilisikika, ingawaje haijabainika ni wahalifu wangapi walihusika kwenye hujuma hiyo. Amedai kuwa, "hatuwezi kusema kwamba wahanga walilengwa kutokana na imani zao za kidini au la."

Hata hivyo Nadeem Sheikh, mwanachama wa Bodi ya Jumuiya ya Waislamu Scarborough amesema ametiwa wasiwasi mkubwa na ufyatuaji risasi huo, na kutoa mwito kwa mamlaka husika kuwafikisha mbele ya sheria waliohusika na jinai hiyo. 

Kundi la wanaume waliokuwa wamemaliza kutekeleza ibada za usiku katika mwezi mtukufu wa Ramadhani katika msikiti ulioko katika wilaya ya Scarborough walimiminiwa risasi na wahalifu waliokuwa kwenye gari.

Maneno ya kibaguzi kwenye kuta za msikiti Canada

Uislamu ni dini inayoenea kwa kasi zaidi Canada ambapo Waislamu wameongezeka kwa asilimia 82 katika kipindi cha muoongo mmoja uliopita. Hivi sasa Waislamu ni karibu asilimia 3.5 ya watu wote milioni 38 nchini Canada. Kutokana na hali hiyo kumekuwepo jitihada za makusudi za kueneza chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.

Waislamu wa Canada hivi sasa wanaishi kwa hofu kutokana na kushtadi visa vya uhalifu na hujuma dhidi yao na matukufu yao. Serikali ya Canada imekuwa ikikosolewa pia kwa kuwawekeka mbinyo Waislamu kupitia sheria zake, kama ya kupiga marufuku vazi la Hijabu.

Tags